BURIANI MOI: Kesi nyingi mahakamani zilimnyima usingizi
Na CHARLES WASONGA
UTULIVU aliotarajia Mzee Daniel Arap Moi baada ya kustaafu ulivurugwa na msururu wa kesi kuhusu ardhi alizodaiwa kunyakua akiwa madarakani.
Mnamo 2003, miezi michache baada ya kuondoka mamlakani, Mzee Moi alishtakiwa na mkulima wa Nakuru, Malcolm Bell kwa tuhuma za kunyakua ekari 100 za ardhi ya familia yake ambako kumejengwa Shule ya Upili ya Moi High School, Kabarak.
Lakini Moi alikanusha madai hayo mbele ya Jaji Muga Apondi akisema babake Bell alimpa ardhi hiyo kama zawadi kwa kumchimbia kisima, kumuunganishia stima na kumjengea josho la ng’ombe.
Katika uamuzi wake, Jaji Apondi alisema kwamba Moi alikuwa na haki ya umiliki wa ardhi hiyo baada ya kuitumia kwa zaidi ya miaka 12.
Bell alipinga uamuzi huo na kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Rufaa ambayo ilibatilisha uamuzi huo wa mahakama kuu.
Katika uamuzi wao, Majaji Martha Koome na Hanna Okwengu walimwamuru Moi aondoke kutika ardhi hiyo.
Walikubaliana na kauli ya Bw Bell kwamba Mzee Moi alichukua ardhi hiyo kinyume cha sheria na kwamba hakutimiza ahadi ya kuwachimbia kisima, kuwawekea stima na josho la ng’ombe.
Mnamo 2013 Mzee Moi alishindwa kubatilisha uamuzi wa majaji wa Mahakama ya Rufaa baada ya majaji watano wa Mahakama ya Juu kudumisha uamuzi wa mahakama hiyo kwamba familia ya Bell ndiyo wamiliki halali wa ardhi hiyo.
Katika aumuzi wao, majaji Kaplana Rawal, Philip Tunoi, Mohammed Ibrahim, Smokin Wanjala na Njoki Ndung’u walisema kuwa uamuzi wa mahakama ya rufaa ulikuwa sawa na haukukiuka kipengee chochote cha Katiba.
Baadaye Bw Bell aliripotiwa katika vyombo vya habari akisema kuwa alikuwa tayari kuruhusu Moi kuendelea kutumia ardhi hiyo mradi waelewane kuhusu malipo.
Mei 2019, Mahakama Kuu ya Eldoret ilimpata Mzee Moi na hatia ya kunyakua ekari 53 za ardhi ya chifu wa zamani Noah Kipngeny Chelugui mjini Eldoret.
Jaji Anthony Ombwayo aliamuru kwamba Moi na usimamizi wa kampuni ya Rai Plywood (K) limited walipe familia ya marehemu Chelugui Sh1 bilioni.
Hii ni baada ya kampuni hiyo inayomilikiwa na familia ya Jaswant Rai kukiri mbele ya mahakama hiyo kwamba Moi ndiye aliwauzia ardhi hiyo mnamo 2007.
Mzee Moi aliwasilisha kesi katika Mahakama ya Rufaa ya Eldoret kupinga uamuzi wa Jaji Ombwayo.
Rais huyo mstaafu pia alikabiliwa na kesi mnamo Julai 2016 aliposhtakiwa kwa kuuza ardhi ya ekari 20 inayodaiwa kuwa mali ya Chuo Kikuu cha United States International University-Africa(USIU-A) jijini Nairobi kwa George Kiongera kwa Sh500 milioni.
Usimamizi wa chuo ulijaribu kurejesha ardhi hiyo kwa kuwasilisha kesi mahakamani pamoja na kufanya maandamano barabarani mnamo Julai 13, 2016. Mvutano huo haujatatuliwa mpaka sasa.
Jina la Mzee Moi pia limetajwa katika kesi ambapo wahusika wawili wanavutania umiliki wa ardhi ya thamani ya Sh1.6 bilioni ambako barabara ya Southern Bypass jijini Nairobi imejengwa.