Habari

#ByElections2025: Wapigakura wachache wajitokeza chaguzi ndogo North Rift

Na WAANDISHI WETU  November 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

IDADI ndogo ya wapigakura ilishuhudiwa katika uchaguzi mdogo wa Seneti kaunti ya Baringo na katika wadi nyingine tatu za North Rift, huku wagombea wakichuana vikali katika kura hizi zinazotajwa kama mwanzo wa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Ukaguzi uliofanywa katika vituo kadhaa vya kupigia kura ulionyesha kuwa wapigakura wachache walijitokeza licha ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kufungua vituo mapema saa moja asubuhi.

Kulikuwa na ulinzi mkali katika vituo vingi huku uthibitishaji wa wapigakura kupitia mfumo wa kielektroniki wa KIEMS ukiendelea bila changamoto kubwa, na hivyo kuwawezesha wananchi kutekeleza haki yao ya kidemokrasia.

Wagombeaji sita wanawania kiti cha Seneti cha Baringo. Miongoni mwao ni Vincent Chemitei wa UDA, Benjamin Chebon wa TND, Shadrack Kibet Kaplawat wa ARC, Steve David Kipruto wa RLP, Samuel Letasio wa Kenya Moja Movement (KMM) na Daniel Kirui wa chama cha Umoja na Maendeleo.

Kufikia nne asubuhi, ni wapigakura 46 pekee kati ya 625 waliokuwa wamepiga kura katika kituo cha Shule ya Msingi ya Tenges. Kwenye Shule ya Msingi ya Tandui ni wapiga kura 12 kati ya 646, huku Timboiywo wakiwa 40 kati ya 676.

Afisa msimamizi wa uchaguzi Hillary Cheburet alihusisha idadi ndogo ya waliojitokeza na shughuli za kila siku.
“Wengi wako mashambani wakivuna mazao, lakini tunategemea watafika kabla ya saa kumi na moja,” alisema.

Kaunti ya Baringo ina jumla ya wapigakura 281,053 walioandikishwa katika vituo 1,029 katika maeneo ya Baringo Central, Eldama Ravine, Baringo North, Baringo South, Tiaty na Mogotio.

Katika Kaunti ya Nandi, wadi ya Chemundu/Kapngetuny pia ilishuhudia idadi ndogo ya wapigakura. Wadi hiyo ina jumla ya wapigakura 14,535 wanaotarajiwa kupiga kura.
“Wengi wamezoea kushiriki Uchaguzi Mkuu, si uchaguzi mdogo,” alisema mkazi, Joshua Kipkemboi.

Kwa mujibu wa afisa msimamizi wa IEBC katika eneo hilo, Rajab Barasa, shughuli ilikuwa ikiendelea vizuri katika vituo 30. Wagombea wa wadi hiyo ni David Kiptoo (Equitable Party), Vincent Rutto (UDA), Shaffie Letting na Robert Kipchirchir wa New Democrats Party.

Huko Turkana, ambapo wapigakura wengi ni wafugaji, idadi kubwa ilijitokeza katika vituo 13 vya wadi ya Nanam, Kaunti Ndogo ya Turkana West.

Kulikuwa na hitilafu ndogo za vifaa vya KIEMS kutokana na joto kali.
“Hamna changamoto kubwa, ni joto tu linaathiri utambuzi,” alisema afisa msimamizi Noah Bowen.

Waangalizi kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa walithibitisha kuwa utaratibu ulikuwa ukiendelea vizuri na makundi maalum yalipewa kipaumbele kupiga kura.

Mgombea wa UDA wadi ya Nanam, Cosmos Longor, aliyepiga kura mapema aliitaka IEBC kuhakikisha uchaguzi ni huru na wa haki.

Katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, hakukuwa na uchaguzi katika wadi ya Metkei baada ya mgombea wa UDA, Philip Kipruto, kutangazwa mshindi na IEBC mnamo Oktoba 29 kwa kukosa mpinzani.
“Nangoja kuapishwa,” alisema Bw Kipruto, aliyewahi kushinda kiti cha wadi hiyo mwaka 2017 akiwa mgombea huru.

Ripoti za Florah Koech, Titus Ominde, Sammy Lutta na Barnabas Bii.