Habari

Chama cha Gachagua kimeiva, tayari kutajwa rasmi Alhamsi – Duru zasema

Na CHARLES WASONGA May 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua Alhamisi, Mei 15, 2026 anatarajiwa kutaja chama cha Democracy for Citizen Party (DCP) kama chombo kipya cha kisiasa anachotarajia kukitumia kulemaza kabisa chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika ngome yake ya Mlima Kenya.

Duru zimeambia Taifa Leo kwamba Bw Gachagua na wandani wake wamekamilisha mipango ya hafla hiyo itakayofanyika katika kaunti ya Nairobi.

Mbunge huyo wa zamani wa Mathira anapania kukitumia chama hicho kuunda muungano mpya wa kisiasa na vyama vingine vya upinzani kwa nia ya kumwondoa mamlaka Rais William Ruto 2027.

“Ndio tuko tayari kwa shughuli muhimu kesho (Mei 15, 2025). Alivyosema bosi wetu chama hicho kipya ni cha kitaifa wala sio cha kikabila au cha eneo la Mlima Kenya inavyodhaniwa,” akasema Mbunge moja wa Nairobi, ambaye ni mwandani wa karibu wa Bw Gachagua.

Lakini mwanasiasa huyo alidinda kutaja mahala mahsusi ambako shughuli hiyo itaendeshwa akisema “hatutaki maadui wetu waharibu hafla yetu.”

Rangi za chama cha DCP ni: kijani, kahawia na nyeusi huku nembo yake ikiwa mkono unaoshika sikio, kuashiria kusikiza kwa makini kile wananchi wanasema.

Aidha, kauli mbiu cha chama hicho ni: “Kazi na Haki”.

Mnamo Jumatano, Mei 14, 2025, wakereketwa wa chama hicho walisambaza mitandaoni picha za bidhaa za chama hicho cha DCP kama vile vitambaa, kofia, tishati miongoni mwa zingine, ishara kwamba wako tayari kwa shughuli ya Alhamisi.

Duru zinasema chama hicho, DCP, kilichosajiliwa Februari 3, 2025, kitazinduliwa rasmi baadaye mwishoni mwa mwezi huu.

Wale ambao wametajwa kama wanachama wa asasi ya uongozi wa chama hicho ni pamoja na; Thomas Ratema, Ado Yiembo, Mably Owino, Hussein Athman, Laura Njeri, Abdifatah Abdullahi, Joyo Gatugi, Jeremiah Mong’eri, Joel Sang, John Maranga, Miriam Fredina Mariki na Brenda Banjira Omusinda.

Hata hivyo, vyeo vyao mahsusi havikubainishwa.

Bw Gachagua, ambaye alijiuzulu rasmi kutoka UDA mnamo Jumatatu Mei 12, 2025 anatarajiwa kukivumisha chama hicho kabla ya kubuni muungano na viongozi wa upinzani kama vike kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa (DAP-K), Martha Karua (People Liberation Party-PLP), aliyekuwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’i, miongoni mwa wengine.