Chanjo mpya ya homa ya matumbo yapokelewa vyema wazazi, watoto wakijazana vituoni
WAZAZI kutoka eneo la Githiogora, eneo bunge la Westlands na eneo bunge la Mathare Kaskazini wametakiwa kujitokeza ili watoto wao walio na umri wa miaka mitano hadi 14 kupewa chanjo mpya ya homa ya matumbo iliyozinduliwa na serikali.
Jumamosi, Waziri wa Afya Aden Duale alizindua chanjo mpya ya homa ya matumbo katika Wadi ya Githongora, kampeni ambayo inalenga watoto milioni 22 ambao wamo hatarini.
Bw Duale alisema kuwa chanjo hiyo aina ya Typhoid Conjugate (TVC) itapewa watoto wenye umri wa miaka kati ya mitano hadi 15. Aliwataka wazazi kutoka kaunti 47 kutoa idhini kwa walimu kuruhusu wahudumu wa jamii kuingia shuleni na kuwachanja watoto hao.
“Chanjo hii ni salama kwa watoto wetu ambao wamo hatarini,” alisema Bw Duale.
Chanjo zingine zilizozinduliwa ni zile za ugonjwa wa ukambi na surua kwa watoto kati ya miezi tisa hadi miaka kumi na 19.
Mkurungenzi wa Afya nchini Daktari Patrick Amoth alisema kaunti 18 zimerekodi visa vya ugonjwa wa ukambi, katika kipindi cha mwaka mmoja watoto 3,000 walipatikana kuwa na ukambi na wengine 18 kufariki.
“Tunapozindua chanjo hapa nchini ni lazima ipitie makundi mawili ya kudhibitisha usalama wake. Kwa hivyo chanjo hii ni salama na mzazi hafai kuwa na wasiwasi.
Katika hospitali ya Level 4, Mathare Kaskazini, wazazi walifurika na watoto wao ili kupata chanjo hiyo.
Afisa wa hospitali hiyo Bw Robert Kariuki alisema kuwa eneo la Ruaka, wanalenga watoto 17,000 kupewa chanjo ya TCV na watoto 22,00 kupewa chanjo ya ukambi katika siku saba zilizosalia.
“Kwa sasa chanjo ya ukambi imetolewa kwa watoto 1,600 na 1,700 kwa chanjo ya homa ya matumbo. Bw Kariuki alisema ili serikali kufikia kiwango hicho, kuna mipangilio mitatu kuhakikisha tunafikia idadi hiyo. Mojawapo ikiwa ni kutumia mbinu ya kufikia wale wazazi na watoto nyumbani.
Bi Winfred Kivai, ambaye alifika katika eneo la Githiogora alisema kuwa kukubali mwanawe kupewa chanjo hiyo ni kutokana na sababu yake kutembelea kituo cha afya mara kwa mara mwanawe kutibiwa maradhi ya homa ya matumbo.
“Niliposikia serikali inazindua chanjo hiyo hapa, niliona ni vyema mwanangu mwenye umri wa miaka kumi na miwili apokee. Homa ya Matumbo ni mbaya sana,” alisema Bi Kivai.
“Nasema ni asante kwa hio chanjo yenye wametuletea, imetusaidia sana itatusaidia ndio watoto wetu wasiugue,” alisema mzazi mwingine Bw Noela Onyango.