Cheti feki cha KCSE: Mbunge Sunkuyia atiwa mbaroni
MBUNGE wa Kajiado Magharibi, George Sunkuyia, amekamatwa na wapelelezi wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kwa kosa la kughushi cheti cha masomo cha Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE).
Mbunge huyo wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) alichukuliwa nyumbani kwake, Nairobi, Jumanne (Mei 27, 2025) asubuhi na kupelekea katika makao makuu ya EACC, jumba la Integrity.
Hii ni kisa cha hivi punde cha mbunge kukamatwa kuhusiana na kosa la kughushi stakabadhi za masomo.
Mbunge wa Juja George Koimburi anakabiliwa na kesi mahakamani kwa kosa hilo hilo.
Aidha, Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi aliwahi kukabiliwa na kesi kuhusiana na kosa kama hilo, lakini kesi hiyo ilitupiliwa mbali na mahakama mwaka jana.
EACC inasema kuwa tangu 2022, imechunguza visa 549 zinazohusiana na watu kughushi stakabadhi za masomo na kitaaluma.
Kati ya visa hivyo, 85 vimewasilishwa kwa afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma na kupelekea watu 13 kupatikana na hatia.