Habari

Chibanzi Mwachonda wa KMPDU augua Covid-19

July 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

KAIMU katibu mkuu wa Chama cha Madaktari Nchini (KMPDU) Dkt Chibanzi Mwachonda amejiunga kwenye orodha ya wahudumu 683 ambao kufikia Ijumaa, Julai 31, 2020, walikuwa wameambukizia virusi vya corona.

Kwenye taaarifa aliyoituma kwa vyombo vya habari Dkt Mwachonda alisema aliambukizwa virusi hivyo akiwa kazini. Lakini alitoa hakikisho kwamba hali yake sio mbaya sana na kwamba amejitenga.

“Familia yangu pia wako salama na hawajaambukizwa. Watu niliotangamana nao wanaendelea kusakwa,” akasema.

Dkt Mwachonda alisema ugonjwa huo umeenea kwa kasi katika jamii na kila Mkenya yuko katika hatari lakini hiyo haipasi kuwa chanzo cha woga au unyanyapaa dhidi ya walioathiriwa au familia zao.

“Idadi kubwa ya wagonjwa wa Covid-19 wanaopimwa inatupa matumaini kwamba, kama taifa, tutashinda vita dhidi ya adui huyu ambaye haonekani,” akaeleza.

Dkt Mwachonda alitoa wito kwa Wakenya kuzingatia masharti ya wizara ya afya kama vil kuvalia barakoa, kunawa mikono, kutotangamana na kutofanya safari zisizo za lazima ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

“Kwa wahudumu wenzangu wa afya nawahimiza kuendelea na kazi ya kuwahudumia wananchi kwa tahadhari kubwa kwani sote tuko katika hatari ya kuambukizwa,” akasema.

Kwa mara nyingine katibu huyo mkuu wa KMDU aliitaka serikali kuendelea kusambaza vifaa vya kujikinga kwa wahudumu wa afya kote nchini marupurupu zaidi na igharimie bima yao ya matibabu.

Kufikia Ijumaa jumla ya wahudumu 683 wameambukizwa Covid-19 wakiwa kazini na wengine wanane (8) wakifariki, akiwemo Dkt Doreen Adisa Lugaliki.