Cop Shakur, mwanajeshi wa zamani kusalia kizuizini kwa kuunda kundi la ‘FBI’
MWANAJESHI wa zamani Patrick Osoi na mlinzi wa zamani wa magereza Jackson Kihara almaarufu Cop Shakur, wataendelea kuzuiliwa rumande hadi wiki ijayo kusubiri uamuzi wa korti kuhusu iwapo wataachiwa kwa dhamana.
Wawili hao wanachunguzwa kwa madai ya kujiandaa kutekekeza uhalifu na kushiriki katika shughuli zinazovuruga utulivu wa umma. Polisi waliomba korti iruhusu wazuiliwe kwa wiki mbili, uchunguzi ukiendelea.
Hakimu wa Mahakama ya Kahawa Gideon Kiage alisema atatoa uamuzi kuhusu ombi hilo Agosti 7, baada ya mawakili wa watuhumiwa kupinga ombi la kutaka wazuiliwe.
Hakimu aliamuru Bw Osoi azuiliwe katika kituo cha polisi cha Muthaiga, huku Bw Kihara, anayejulikana kama ‘Cop Shakur’, akizuiliwa kituo cha polisi cha Pangani.
Ukipinga wawili hao kuachiliwa kwa dhamana, upande wa mashtaka ulisema kwamba watuhumiwa hao wana ushawishi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, ambapo wana wafuasi wengi.
Korti iliambiwa kwamba wawili hao wanaweza kuwasiliana na wafuasi wao kwa njia zinazoweza kuzuia haki.
Upande wa mashtaka pia ulidai kwamba kuachilia watuhumiwa hao kwa sasa kunaweza kuvuruga ushahidi muhimu na kutishia mashahidi.
“Washtakiwa wana uwezo wa kuingilia uchunguzi na mashahidi. Kuachiliwa kwao kunaweza kusababisha kufutwa kwa machapisho yanayofanya wachunguzwe na kuharibu ushahidi muhimu wa kidijitali,” alisema kiongozi wa mashtaka.
Katika hati ya kiapo, Inspekta mkuu Josephine Korir alisema kwamba walipokea taarifa Julai 28, 2025, kwamba Bw Osoi alikuwa akiandaa vita dhidi ya maafisa wa polisi wenye sare.
Aliongeza kwamba mtuhumiwa huyo alikamatwa Julai 29 kwa tuhuma ya kushiriki katika shughuli zinazoharibu utulivu wa umma, usalama wa taifa, na udumishaji wa amani kabla, wakati, na baada ya maandamano ya Juni 25, 2025, na Julai 7, 2025.
Afisa huyo wa uchunguzi alisema kwamba Bw Osoi, kupitia akaunti yake ya X, alitangaza kuunda kikundi cha Fighting Brutality Initiative (FBI) na kuwaajiri maafisa wa polisi wa zamani na wa sasa ili kupigana na maagizo yasiyo halali.
Kulingana na afisa huyo, chapisho hilo lilileta matatizo makubwa ya usalama wa taifa, na kuongeza kwamba chapisho hilo la mitandao ya kijamii kuhusu kikundi hicho lilivutia maoni.
TAFSIRI: BENSON MATHEKA