CORONA: Mawaziri hawana muda wa wananchi
Na BENSON MATHEKA
MAWAZIRI watatu Jumanne walikataa kufika mbele ya kamati ya pamoja ya afya ya Bunge la Taifa na Seneti kueleza kuhusu matayarisho yaliyofanywa na serikali kuzuia na kukabiliana na virusi vya corona iwapo vitazuka nchini.
Kamati hiyo ilikuwa imewaalika mawaziri Mutahi Kagwe (Afya), Fred Matiang’i (Usalama) na James Macharia (Uchukuzi) kuwapa Wakenya habari kuhusu hatua walizochukua tangu Rais Uhuru Kenyatta alipotoa maagizo kuhusu maandalizi ya kuzuia na kupambana na virusi hivyo nchini wiki iliyopita.
Rais Kenyatta alitoa agizo hilo kufuatia shinikizo kutoka kwa vyombo vya habari na wananchi hasa kuhuru kuruhusiwa nchini kwa raia 239 kutoka China bila kuhakikisha wako salama.
Virusi hivyo vimezua wasiwasi kote duniani vikiendelea kusambaa katika mataifa zaidi tangu vilipozuka China mwishoni mwa mwaka jana.
Wanachama wa kamati hiyo iliyosimamiwa na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Murang’a, Sabina Chege walisema inasikitisha kuwa mawaziri hao waliamua kupuuza kikao cha kujadili suala lenye umuhimu mkubwa la virusi vya corona.
“Hii ilikuwa fursa ya mawaziri na wataalamu katika wizara zao kueleza Wakenya hatua zilizochukuliwa na serikali, na wanayopaswa kutarajia kwa sababu kuna hofu kuhusu virusi vya corona. Kwa kukosa kufika, ni wazi wanaidharau kamati hii na Wakenya kwa jumla,” akasema Mbunge wa Kimilili Dkt Eseli Simiyu.
Wakijadili hoja ya kuahirisha kikao hicho, wanachama hao walisema kuwa kutofika kwa mawaziri hao kutoa habari kwa Wakenya kunaonyesha hakuna yeyote serikalini anayetaka kuwajibika iwapo virusi vya homa hiyo hatari vitaingia nchini.
“Hili ni suala muhimu linalohitaji mawaziri wenyewe kufika mbele ya kamati hii, wala sio kuwatuma wasaidizi wao. Wakenya wana maswali wanayotarajia majibu yake kupitia kikao hiki,” akasema Seneta wa Nyamira Okong’o Omongeni.
Kulingana na wanakamati hao, mawaziri hao hawakufaa kuwasilisha majibu na maelezo kupitia maandishi pekee bali walipaswa kufika mbele ya kamati ili kufafanua jinsi serikali inavyoshughulikia suala la virusi vya corona.
Wanachama hao walikataa barua kutoka kwa wizara husika zilizoeleza kwamba mawaziri hao walikuwa na shughuli tofauti za kikazi, wakisema hakuna kazi iliyo na dharura kwa sasa kuliko virusi vya corona.
Pia walikataa kuwasikiza maafisa waliotumwa na mawaziri hao kuwaakilisha. Bw Kagwe alimtuma waziri msaidizi kumwakilisha, Bw Macharia alimtuma katibu wa wizara naye Bw Matiang’i alimtuma mkurugenzi wa uhamiaji.
“Hofu imetanda nchini na Wakenya walitarajia kupata maelezo kupitia kikao hiki. Hakuna shughuli iliyo muhimu kuliko hii kwa sababu virusi vya corona vinaweza kusimamisha kazi zingine zote iwapo vitazuka nchini,” akasema Seneta Maalum Beth Mugo.
Miongoni mwa maswali ambayo wabunge walitaka mawaziri hao kujibu ni iwapo raia 239 wa China waliowasili nchini wiki jana wametengwa katika kambi ya kijeshi kama ilivyoagizwa na mahakama.
Mnamo Jumapili, Waziri Kagwe alisema hakukuwa na haja ya agizo hilo la mahakama kwa sababu serikali ilikuwa imeweka mikakati ya kufuatilia abiria hao.
Bw Kagwe alisema hofu ya maradhi hayo imetiliwa chumvi akisema virusi hivyo sio hatari kama inavyodaiwa na mataifa mengine duniani, mashirika ya afya na vyombo vya habari.
Maswali mengine ambayo mawaziri hao wangeulizwa ni kuhusu hali ya raia wa Kenya walio China hasa wanafunzi 100 walio jiji la Wuhan, ambako maradhi hayo yalianzia na kwa nini iliruhusu raia wa kigeni wanaoingia nchini kujitenga wenyewe.
Katika kile ambacho kinaonekana kama kuficha habari kuhusu maradhi hayo, Serikali pia imetisha kuwachukulia hatua Wakenya wakisambaza habari kuhusu hofu ya kuwepo kwa maradhi hayo nchini.