CORONA: Serikali yapuuza agizo la kutenga abiria kutoka China
Na CHARLES WASONGA
SERIKALI ilikiri Jumatano kuwa haijatimiza agizo la mahakama lililoitaka kuwatenga abiria 239 waliotoka China wiki jana katika kambi ya jeshi, kama tahadhari ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona nchini.
Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani Karanja Kibicho, aliiambia Kamati ya Pamoja ya Bunge la Kitaifa na Seneti kuwa serikali haijaweza kuwasaka abiria hao kama korti ilivyoagiza.
“Hatujaweza kutimiza agizo la mahakama la kuwatenga abiria hao katika kambi za KDF. Lakini ninataka kuihakikishia kamati hii kwamba abiria wote 239 waliowasili nchini kutoka China hawana virusi vya corona. Tumepata hakikisho hili kutoka kwa Wizara Afya,” akasema Bw Kibicho.
Katibu huyo ambaye ni mwanachama wa jopokazi lililobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta kuongoza juhudi za kuzuia na kukabili maambukizi ya corona, aliwataka Wakenya wasiwe na hofu kuhusu abiria hao.
“Ijapokuwa hatuwakamata na kuwapeleka katika kambi za KDF, Wizara ya Afya ina maelezo kuhusu kila mmoja wa watu hao,” akasema.
Dkt Kibicho alikuwa akitoa taarifa kwa kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Murang’a Sabina Chege na Seneta wa Trans Nzoia Michael Mbito.
Ijumaa iliyopita, Jaji James Makau alimwagiza Waziri wa Usalama Fred Matiang’i awasake na kuwapeleka abiria hao katika kambi za jeshi kwa siku 14, hadi ithibitishwe hawana virusi hivyo.
Chama cha Mawakili (LSK), kile cha madaktari na mwanaharakati mmoja, walikuwa wameshtaki serikali wakitaka isitishe safari za ndege kutoka China.
Dkt Kibicho aliandamana na Waziri wa Uchukuzi James Macharia, ambapo walitoa sababu za Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kutofika mbele ya kamati hiyo Jumanne.
Bw Macharia alisema kufikia sasa safari zote za ndege kutoka Kenya hadi China zimesimamishwa, pamoja na kupiga marufuku safari za kuelekea maeneo fulani ya Italia ambako visa vya virusi vya corona vimeripotiwa.
“Kando na hayo tumeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa wageni wanaoingia nchini kupitia maeneo mengine ya mipaka wanakaguliwa. Tumeagiza mamlaka ya Safari za Angani Nchini (KCAA) kukagua ndege zote zinazoingia nchini,” akasema.
Kamati hiyo ya bunge iliagiza kwamba Bw Kagwe afike mbele yake leo alasiri.