CORONA: Tahadhari kwa abiria
Na WANDERI KAMAU
SERIKALI imetoa kanuni kali kwa abiria na wadau katika sekta ya matatu kuzingatia tahadhari ili kudhibiti maenezi ya virusi vya corona wanaposafiri.
Waziri wa Uchukuzi, Bw James Macharia alisema kuwa magari hayo yanapaswa kuacha mtindo wa kuwabeba abiria kupita kiasi, ili kutohatarisha maisha ya wale ambao imewabeba.
Kanuni hizo pia zitazingatiwa na magari ya moshi yanayowasafirisha kutoka mitaa mbalimbali hadi jijini Nairobi.
Akiwahutubia wanahabari katika kituo cha matatu cha Railways jijini Nairobi jana, Bw Macharia alisema kuwa maafisa wa wizara hiyo watakuwa katika sehemu mbalimbali nchini kuhakikisha kuwa kanuni hizo zimezingatiwa.
“Ingawa hatua hii inalenga kubuni ushirikiano mzuri na sekta ya matatu, maafisa wetu watakuwa katika vituo mbalimbali nchini kuhakikisha kuwa kanuni hizo zimezingatiwa. Ni muhimu kwa abiria kushirikiana nasi kuhakikisha kuwa tumeungana kwenye vita hivi,” akasema Bw Macharia.
Wenye magari watatakiwa kuyaosha magari yao kila baada ya kuwabeba abiria, ili kupunguza uwezekano wa virusi kuwepo katika magari hayo.
Hii ni kinyume na kawaida, ambapo magari mengi huoshwa mara moja ama mbili kwa siku.
Kando na hayo, Bw Macharia alisema kuwa ni lazima magari hayo yawe na dawa za kutosha za kuua viini hivyo ili kuhakikisha kuwa abiria wanaosafiri wako salama.
Hata hivyo, wadau hao walilalamikia uhaba na bei ya juu ya dawa hizo, wakisema kuwa serikali inapaswa kuingilia kati kuhakikisha kuwa zinapatikana kwa urahisi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Matatu (MOA), Bw Simon Kimutai, alisema kuwa ni lazima Wizara ya Afya ipunguze bei ya dawa hizo, ama izisambaze kwa steji mbalimbali za matatu ili kuhakikisha kuwa kila gari imepata.
“Hali ilivyo, ni vigumu sana kwetu kupata dawa za kutosha kwani hazipo katika maduka mengi,” alisema Bw Mbugua, kwenye kauli iliyoungwa mkono na mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Maslahi ya Wenye Matatu (MWA), Bw Dickson Mbugua.
Akaongeza, “Vile vile, zinauzwa kwa bei ya juu sana. Hivyo, itakuwa vizuri kwa serikali kuhakikisha kuwa zinapatikana kwa urahisi ili kuhakikisha tunazingatia usafi wa kutosha katika magari yetu.”
Vile vile, aliwataka makondakta kutumia njia ya M-Pesa kuwatoza abiria nauli ikiwezekana, ikizingatiwa kuwa virusi hivyo pia vinaambukizwa kwa njia ya watu kugusana.
Na kutokana na kupungua kwa kiwango cha abiria, Bw Mbugua alizitaka benki kuwapunguzia masharti wenye matatu ambao wanalipia mikopo yao.
Maelfu ya Wakenya hutumia matatu kwenda kazini, na huwa mojawapo ya sekta muhimu katika ukuaji wa nchi.
Wakati huo huo Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri Salama Barabarani (NTSA) imesimamisha kwa muda utoaji leseni za kisasa za uendeshaji magari.
Hata hivyo, mamlaka ilisema kuwa itatuma arafa kwa wale ambao walikuwa wametuma maombi ya kupata leseni hizo kuwafahamisha kuhusu hatua hiyo.
Huduma zingine zilizosimamishwa kwa muda ni utoaji wa stakabadhi za umiliki wa magari, nambari za usajili wa magari na vibandiko vya magari ya usafiri wa umma.