Habari

CORONA: Watu 23 wafariki

August 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Afya Mutahi Kagwe ameelezea hofu kuhusu ongezeko la idadi ya vijana wanaofariki kutokana na Covid-19 huku Kenya ikiandikisha idadi ya watu 23 waliofariki ndani ya muda wa saa 24.

Idadi hiyo ya vifo ni ya juu zaidi kuwahi kuripotiwa nchini ndani ya muda wa siku moja tangu mrukurupuko wa janga hili uripotiwe Kenya kwa mara ya kwanza mnamo Machi 13, 2020.

Kwa hivyo kufikia Jumamosi, Agosti 1, 2020, jumla ya watu 364 walikuwa wamefariki nchini baada ya kuathiriwa na virusi vya corona.

Akiongea na wanahabari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) waziri Kagwe pia amethibitisha visa vipya 727 vya maambukizi ya virusi vya corona baada ya sampuli 6,371 kuchunguzwa.

Hii inafikisha 21,363 idadi jumla ya maambukizi nchini. Kati ya wagonjwa hao wapya 696 ni Wakenya ilhali 31 ni raia wa kigeni.

Mwenye umri mdogo zaidi ni mtoto wa umri wa mwaka mmoja naye mwenye umri mkubwa zaidi ni mzee mwenye umri wa miaka 92.

“Inasikitika kuwa miongoni mwa wagonjwa 23 waliofariki, kuna msichana mwenye umri wa miaka 16 ambaye hakuwa na matatizo mengine ya kiafya hapo awali. Hii ina maana kuwa vijana sasa wako katika hatari kubwa ya kuangamizwa na adui huyu,” akasema Bw Kagwe.

Waziri ametangaza habari njema kwamba jumla ya wagonjwa 254 walipona, 88 kati yao walikuwa wakiuguzwa nyumbani huku 166 walikuwa wakihudumiwa katika hospitali mbalimbali.

Kaimu Mkurugenzi wa Afya Patrick Amoth alisema miongoni mwa sababu za wagonjwa wengi kufariki ni kwamba walifika hospitalini kuchelewa.

“Unaweza kuwa umeambukizwa Covid-19 bila wewe kufahamu. Wengine huhisi vibaya lakini wanahofia kwenda hospitalini. Ni muhimu mgonjwa yeyote kutafuta matibabu ya haraka,” akasema Dkt Amoth.

Kati ya visa vipya, 470 vinatoka kaunti ya Nairobi, Kiambu (64), Kajiado (25), Kirinyaga (20), Mombasa (16), Migori (15), Busia (13), Machakos (12), Laikipia (11), Nakuru (9), Murang’a (9) na Kisumu (9).

Kaunti zingine ziliandikisha visa vya maambukizi ni; Nyeri (7), Siaya (7), Nyandarua (5), Uasin Gishu (5), Narok (5), Isiolo (4), Nandi (4), Garissa (3), Bomet (2), Meru 2. Vihiga (2), Homa Bay (2) huku kaunti za Kilifi, Bungoma, Kisii, Samburu, Tran-Nzoia, na Kwale vikiandisha kisa kimoja kila moja.