Habari

Corona yaruka reggae ikinoga

October 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

KUNA hofu kwamba huenda wanasiasa sasa wakaibuka kuwa maajenti wakuu wa kusambaza virusi vya corona nchini huku wimbi jipya la maambukizi likishuhudiwa nchini.

Tangu Rais Uhuru Kenyatta awaruhusu Wakenya kurejelea baadhi ya shughuli za kiuchumi mwishoni mwa Septemba, maambukizi ya virusi hivyo yamekuwa yakiongezeka karibu kila siku kinyume na ilivyokuwa awali.

Upeo wa maambukizi hayo ulikuwa Alhamisi, baada ya Wizara ya Afya kutangaza visa 1,068 vya maambukizi, hiyo ikiwa idadi ya juu zaidi kutangazwa kwa siku moja tangu virusi vilipogunduliwa nchini mnamo Machi.

Hofu zaidi inatokana na ukiukaji wa wazi wa kanuni za kudhibiti maambukizi unaoendeshwa na wanasiasa wakuu nchini, wakiwemo Rais Kenyatta, Naibu Rais William Ruto kiongozi wa ODM, Raila Odinga kati ya wengine.

Mnamo Alhamisi, Rais Kenyatta na Bw Odinga walifanya mikutano kadhaa ya uzinduzi wa miradi ya maendeleo jijini Kisumu, ambako walipokewa kwa shangwe na maelfu ya wenyeji.

Wawili hao walitumia mikutano hiyo kuipigia debe ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), huku wakati mwingine wakitekwa na mbwembwe za wafuasi wao kwa kushiriki densi na nyimbo za kuivumisha ripoti hiyo maarufu kama reggae.

Kwenye mikutano hiyo, hakuna hata mmoja aliyeonekana kujali hatari iliyowakumba kwa kutozingatia kanuni za kudhibiti maambukizi kama kutokaribiana ama kuvali barakoa.

Ijumaa, Rais Kenyatta pia aliwahutubia mamia ya watu waliojitokeza baada ya kukutana na wahudumu wa Bodaboda katika Ukumbi wa Kijamii wa Pumwani, ulio katika mtaa wa Majengo, jijini Nairobi.

Dkt Ruto vile vile alikutana na ujumbe wa viongozi kadhaa kutoka Kaunti ya Wajir katika makazi yake mtaani Karen, Nairobi, kwenye hatua inayoonekana kuendeleza kampeni yake kuwania urais mnamo 2022.

Hayo yote yanaendelea huku Wizara ya Elimu ikipuuzilia mbali uwezekano wowote wa shule kufungwa tena.

Akihutubu Ijumaa katika Kaunti ya Kakamega, Waziri wa Elimu Prof George Magoha, alisema wanashirikiana kwa karibu na wizara za Afya na Usalama wa Ndani kutathmini mkondo wa maambukizi ya virusi tangu wanafunzi wa Gredi ya Nne, Darasa la Nane na Kidato cha Nne kurejelea masomo yao wiki mbili zilizopita.

“Tunafuatilia kwa karibu mkondo wa maambukizi tangu watoto wetu warejee shuleni. Hatutafunga shule kwani visa vilivyoripotiwa katika shule kadhaa vimetokea katika sehemu tofauti. Tutatoa mwelekeo kuhusiana na maambukizi hayo,” akasema.

Kauli ya waziri ilijiri huku shule mbili za upili zikifungwa katika Kaunti ya Mombasa, baada ya walimu na wanafunzi kuthibitishwa kuambukizwa virusi hivyo. Shule ya Upili ya Wasichana na Star of the Sea na ile ya Tononoka zililazimika kufungwa kwa majuma mawili mnamo Jumatatu, ili kudhibiti maambukizi zaidi kutokea.

Jumapili, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alionya kuwa huenda Kenya ikajipata kwenye wimbi la pili la maambukizi hayo, akiwalaumu wanasiasa kama chanzo kikuu cha ongezeko la maambukizi mapya.

“Hili ni suala lenye uzito. Tunapaswa kuzingatia kanuni zilizotolewa kuepuka mchipuko wa wimbi la pili la maambukizi,” akasema.