Habari

Corona yatimua watu ofisini, wengi wasafiri mashinani

March 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na WAANDISHI WETU

KAMPUNI za kibinafsi na mashirika ya serikali, sasa yameanza kuagiza wafanyakazi wao kufanyia kazi nyumbani huku wasio na ajira wakisafiri mashambani.

Wafanyakazi wengine wakipewa likizo na baadhi yao kusimamishwa kazi katika juhudi za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Mnamo Jumapili, Rais Uhuru Kenyatta alishauri wakuu wa kampuni na taasisi za serikali kuruhusu wafanyakazi kutoa huduma bila kwenda afisini.

Rais pia aliamuru kufungwa kwa shule zote na vyuo. Hii imelazimu maelfu ya walimu na wahadhiri kwenda nyumbani wakisubiri maagizo zaidi kutoka kwa serikali.

Jumanne, wabunge, maseneta na wafanyikazi wa Bunge la Taifa na Seneti walielekea nyumbani baada ya taasisi hizo kusimamisha vikao hadi Aprili 14.

Maelfu ya majaji, mahakimu, waendesha mashtaka na makarani wa mahakama pia wako nyumbani baada ya Jaji Mkuu David Maraga kuagiza kusitishwa kwa huduma nyingi za idara hiyo.

Hapo jana, Mahakama za Makadara na Kibera jijini Nairobi zilikuwa zimefungwa. Wafanyakazi wachache waliokuwepo ni wale ambao walikuwa wakipokea malipo ya dhamana.

Katika Mahakama ya Milimani, kesi tatu zilisikizwa katika eneo la kuegesha magari chini ya usimamizi wa Hakimu Mkazi Muthobi Nzibe.

Jaji David Maraga alikuwa ameagiza kesi zisizo za dharura na zile ambazo sio za uhalifu zisitishwe kwa muda, huku polisi wakihitajika kutatua masuala mengine ya utovu wa kisheria vituoni.

Madiwani kote nchini pia wamefunga ofisi kufuatia ushauri wa Baraza la Mabunge ya Kaunti. Katibu Mkuu wa baraza hilo Kipkurui Chepkwony, alisema hatua hiyo itadumu kwa siku 15.

“Baada ya maambukizi ya virusi vya corona kutambuliwa nchini, tumetambua hili ni suala zito linaloweza kuhatarisha maisha ya madiwani na wafanyakazi. Kwa hivyo vikao vyote nchini vimesimamishwa,” akasema.

Katika afisi kuu za kaunti, baadhi ya magavana waliamua kuagiza wafanyakazi wengi kwenda likizoni kwa muda wengine wakihudumu kutoka nyumbani. Mfano ni kaunti za Pokot Magharibi, Nandi na Siaya ambapo maelfu ya wafanyakazi waliagizwa kutoenda afisini.

Wale watakaotakikana kuendelea na kazi afisini mwao ni wafanyakazi ambao hutoa huduma muhimu kama vile za afya, usalama na usafi.

“Mawaziri wa kaunti, maafisa wakuu na wakurugenzi wa idara wanahimizwa kuandaa ratiba ya kazi, ili wafanyakazi ambao wanawasimamia wawe wakihudumu kwa zamu kwa siku 14 zijazo,” akasema Gavana wa Siaya Cornel Rasanga.

Wakuu wa kaunti kama vile Kisii pia waliagiza masoko makubwa yafungwe. Hali hii italazimu wauzaji kukaa nyumbani au watafute mbinu nyingine za kujichumia riziki.

Wizara ya Ardhi nayo iliamua kufunga afisi zake zote nchini kwa siku 30. Kupitia kwa taarifa, wizara hiyo ilisema lengo ni kulinda wafanyakazi na umma kwa jumla dhidi ya maambukizi ya corona.

Kampuni za kibinafsi yakiwemo mashirika ya habari, hoteli na benki pia ziliamua kupunguza idadi ya wafanyakazi watakaohitajika afisini.

Katika sekta ya utalii, hoteli kadhaa ziliagiza baadhi ya wafanyakazi kwenda nyumbani kwa muda kwani ni mojawapo ya sekta zilizoathirika zaidi na mkurupuko wa corona.

Maagizo ya kufunga vilabu na fuo za Pwani ya Mombasa pia yamefanya wafanyakazi wanaotegemea biashara hizo kukaa nyumbani.

Katika Kaunti ya Nakuru, Mkurugenzi wa hoteli ya Eagle Palace Ibrahim Osman, aliwaambia waandishi wa habari kwamba hali inaendelea kuwa mbaya.

“Tulikuwa tuwe na vikao vinne vya mikutano hapa, lakini vyote vikaahirishwa kwa sababu ya virusi vya corona. Biashara imeharibika. Ni kwa sababu hiyo ndipo tuliamua kuwasimamisha kazi zaidi ya wafanyikazi 25 hadi pale hali itakapoimarika,” akasema Bw Osman.

Wakulima hawajasazwa, hasa wanaotegemea soko la kigeni kwani wameanza kukosa pa kuuza mazao yao na hivyo kuwapelekea wengi kukosa kazi.

“Soko letu kubwa ni China na Ulaya, ambazo zina idadi kubwa ya maambukizi ya corona. Athari pia imetokana na agizo la kuzuia usafiri katika nchi ambazo zimepata wagonjwa,” akasema aliyekuwa Mkuu wa Benki Kuu ya Kenya Micah Cheserem, ambaye ni mkulima mkubwa wa parachichi na maua.

Ripoti za: Valentine Obara, Richard Munguti, Onyango K’Onyango, Joyline Cheplemboi, Samuel Baya na Oscar Kakai