Corona yaua mbunge, marais wakiugua
WAANDISHI WETU na MASHIRIKA
HUKU maafisa wa serikali ya Kenya wakionesha utepetevu katika kukabiliana na homa ya Corona, makali ya maradhi hayo yanaendelea kutikisa viongozi wa nchi mbalimbali duniani bila kujali hadhi wala tabaka.
Kama thibitisho kuwa ugonjwa huo hautambui na kuheshimu tabaka, mbunge Mohammad Ali Ramazani wa Iran alifariki baada ya kuugua kwa siku kadhaa.
Wakati janga hilo likiendelea kuitikisa dunia, viongozi wakuu wa serikali humu nchini wamelaumiwa pakubwa kwa kuonyesha ulegevu kwenye harakati za kuukabili ugonjwa huo.
Mawaziri Reychelle Omamo (Mashauri ya Kigeni), Dkt Fred Matiang’i (Usalama wa Ndani), Sicily Kariuki (Waziri wa Afya anayeondoka) na James Macharia (Uchukuzi) wamejipata lawamani kuhusu mikakati ambayo Kenya imechukua ili kuzuia virusi hivyo kuingia nchini.
Kuingia kwa maradhi hayo Kenya kunaweza kusababisha janga la kitaifa ambalo halitasaza yeyote wakiwemo viongozi wa wakuu jinsi ilivyofanyika Iran ambako Naibu Rais Masoumeh Ebtekar amewekwa mahali palipotengwa baada ya kuthibitishwa kuambukizwa virusi hivyo.
Naibu Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Iraj Harirchi, pia ametengwa baada ya kubainika kuwa aliambukizwa homa hiyo.
Rais Battulga Khaltmaa wa Mongolia pia ametengwa baada ya kurejea nchini humo kutoka China. Rais Khaltmaa alitengwa pamoja na maafisa wengine katika serikali yake, siku moja baada ya kurejea nchini mwake kutoka China.
Kwenye ziara hiyo ya Alhamisi, alikuwa ameandamana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni Tsogtbaatar Damdin, na maafisa wengine wa ngazi za juu.
Kulingana na shirika la habari la Iran, ISNA, mbunge Ramazani alifariki baada ya “kulazwa hospitalini kutokana na matatizo ya kupumua.”
Mashirika ya habari nchini humo yalisema kuwa mbunge huyo alikuwa miongoni mwa wabunge watano ambao walikuwa wamethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo.
Hali yake iliripotiwa kuwa mbaya, kwani hakuonyesha dalili zozote za kupata nafuu.
Hofu ilizidi nchini baada ya ndege ya Shirika la Ndege la Southern China Airlines kutua katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) mapema wiki hii ikiwa na abiria 239.
Kuanzia Alhamisi, Wakenya waliongeza shinikizo kwa Serikali, wakilalama kwamba “inacheza na maisha yao”. Baadhi yao walilalamika kuwa maafisa wa serikali wanachukulia maradhi hayo kama mzaha tu.
Ghadhabu zilizidi hasa baada ya Bi Omamo kutowaridhisha wabunge kuhusu sababu ambazo ziliifanya ndege hiyo kuruhusiwa kuwasili nchini, ikizingatiwa kuwa kuna wanafunzi na Wakenya karibu 100 ambao wamekwama China na serikali imekataa kuwarejesha nyumbani.
Haya yanajiri huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likionya “kushangazwa” na kasi ya kusambaa kwake.
Shirika hilo pia limeonya kuwa huenda maradhi hayo yakageuka kuwa janga kubwa zaidi, ikiwa yatabisha hodi katika nchi za bara Afrika.
Hii ni kwa kuwa mataifa mengi ya bara hili hayana mifumo thabiti kiafya kudhibiti majanga kama hayo.
Tayari, visa vya maambukizi vimeripotiwa Nigeria, Algeria na Misri.
Kufikia Jumamosi, watu 85,705 walikuwa wamethibitishwa kuambukizwa huku watu 2,933 wakifariki katika nchi 61 kote duniani.
Barani Afrika, Algeria na Nigeria zimeripoti kuingia kwa maradhi hayo nchini mwao.
Bi Omamo alifika mbele ya Kamati ya Bunge Kuhusu Ulinzi na Mahusiano ya Nje mnamo Alhamisi, kuelezea mikakati ya serikali kuhusu Wakenya ambao bado wamekwama China.
Waziri Macharia anaelekezewa kidole cha lawama, kuhusu mikakati ya usafiri ambayo imewekwa kuhakikisha kuwa kuna uakguzi wa kutosha kwa raia wa kigeni ambao wanawasili nchini kutoka ughaibuni.
Hilo pia lilimfanya Rais Uhuru Kenyatta kutoa amri kwa Wizara ya Afya kubuni sehemu ya kutosha kuwatenga watu wanaopatikana na virusi vya ugonjwa huo katika Hospitali ya Mbagathi, Nairobi na hospitali zote za kiwango cha Level Five kote nchini.