HabariSiasa

Corona yazima kelele za siasa

March 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

RIPOTI kuhusu kisa cha kwanza cha maambukizi ya virusi vya corona wiki jana, zilituliza ghafla kelele za kisiasa nchini baada ya mikutano ya hadhara kufutiliwa mbali.

Wanasiasa waliokuwa wakilumbana, hasa kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI), kura ya maamuzi na siasa za urithi za 2022 katika mikutano hiyo walinyamaza kwa kukosa majukwaa ya kuendeleza siasa.

Kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto ambao walikuwa wakiongoza wafuasi wao kurushiana lawama walitulia.

Kabla ya Alhamisi wiki jana, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alipotangaza kuwa kisa cha kwanza cha virusi vya corona kilikuwa kimethibitishwa nchini, wafuasi wa viongozi hao walikuwa wakishambuliana kuhusu mkutano wa BBI uliopangiwa kufanyika mjini Nakuru, Jumamosi ijayo.

Kauli ya mwisho ya wandani wa Dkt Ruto ilikuwa onyo kwa Bw Odinga na wandani wake kwamba, hawangeruhusiwa kuzungumza katika mkutano huo, wakisema ulikuwa wa kujadili masuala ya eneo la Rift Valley.

Rais Kenyatta alikuwa amekutana na magavana wa eneo hilo katika juhudi za kutuliza joto kuhusu mkutano huo na kuwaeleza kwamba, alikuwa na imani na Bw Odinga kuongoza mchakato wa BBI.

Mbali na kupiga marufuku mikutano ya hadhara nchini ili kuzuia mambukizi ya corona, serikali imesimamisha mikutano ya mazishi ambayo wanasiasa hutumia kuendeleza siasa.

Serikali imeagiza familia kuzika wapendwa wao bila kualika umati wa watu, hatua ambayo imenyima wanasiasa jukwaa muhimu la kushambuliana.

“Virusi vya corona vimekuwa pigo kwa wanasiasa ambao sasa hawana majukwaa ya kutumia kushambuliana. Nchi imetulia, niko na hakika kama corona haingethibitishwa nchini siasa zingekuwa zimechacha,” asema Brian Githome, mwanathiolojia wa kanisa la Free Pentecostal Fellowship.

Anasema jukwaa lingine ambalo wanasiasa wamekuwa wakitumia ni makanisa ambayo yalirekodi idadi ndogo ya waumini wikendi iliyopita.

Viongozi wa makanisa wamehimiza waumini kufuatilia ibada kutoka nyumbani iwapo wanahisi kuwa wagonjwa. Jumapili iliyopita makanisa yalikuwa na idadi dogo ya waumini na wanasiasa hawakupata jukwaa la kuzungumzia siasa.

Dkt Ruto ambaye amekuwa akitumia ibada makanisani kukosoa wapinzani wake wa kisiasa alitumia mtandao wa Twitter kuhimiza Wakenya kuomba tofauti na awali alipokuwa akikosoa vyombo vya habari kwa kuandika habari za kukosoa kampeni zake za mapema za uchaguzi wa 2022.

“Hata tunapokabili changamoto la coronavirus, tukumbushane maandiko, Kitabu cha Pili cha Nyakati 7: 14.”