COVID-19: Kenya yafikisha visa jumla 88,380 idadi ya vifo ikifika 1,526
Na CHARLES WASONGA
WIZARA ya Afya ilitangaza Jumapili kuwa jumla ya wagonjwa wanane wamefariki huku visa 396 vipya vya maambukizi vikinakiliwa kote nchini.
Kwa hivyo, kufikia wakati huo idadi jumla ya vifo ni 1,526.
Visa hivyo vipya vya maambukizi vilithibitishwa baada ya sampuli kutoka kwa watu 4,717 kupimwa ndani ya muda wa saa 24 kufikia wakati wa kutumwa kwa ripoti kwa vyombo vya habari na hivyo kupandisha idadi jumla ya sampuli zilizopimwa tangu Machi 13 kuwa 931,799. Idadi jumla ya maambukizi ya corona nchini nayo ni 88,380.
Kulingana na taarifa kutoka kwa wizara hiyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari, jumla ya wagonjwa 1,178 wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini huku wengine 8,113 wakitunzwa chini ya mpango wa uuguzi nyumbani.
“Vile vile, jumla ya wagonjwa 86 wamelazwa katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi ilhali wengine 49 wanaongezwa hewa ya oksijen,” ikasema taarifa ikasema.
Kaunti ya Nairobi kwa mara nyingine imeongoza kwa visa vipya vya maambukizi kwa kuandikisha visa Kiambu (40), Busia (31), Bungoma (30), Mombasa (23), Murang’a (19), Nakuru (14), Garissa (14), Kakamega (12), Nyeri (8), Kirinyaga (7), Kisumu (6),Vihiga (6), Laikipia (5), Migori (5), Makueni (4), Embu (4), Meru (3), Kajiado (2), Machakos (2), Kericho (2), Narok (2).
Vile vile, kaunti za Kilifi, Kisii, na Uasin Gishu kila moja imenakili kisa kimoja cha maambukizi ya corona.
Habari njema ni kwamba jumla ya wagonjwa 397 walithibitishwa kupata afueni na kuruhusiwa kurejelea maisha yao ya kawaida ambapo 318 walikuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali huku 79 wakiuguzwa chini ya mpango wa utunzaji nyumbani.