Habari

COVID-19: Rais Kenyatta asisitiza uadilifu sekta ya biashara

March 18th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

WAFANYABIASHARA wakiritimba na wenye tamaa kuongeza bei za bidhaa wakati huu taifa na dunia nzima inapambana na janga la Covid -19 wataadhibiwa vikali, ameonya Rais Uhuru Kenyatta.

Rais amesema Jumatano ni ukosefu wa utu kwa mfanyabiashara yeyote pamoja na maduka kuongeza bei za bidhaa kipindi hiki taifa linapitia ugumu kufuatia maambukizi ya virusi hatari ambavyo mara ya kwanza viliripotiwa mjini Wuhan katika mkoa wa Hubei, China.

Imeibainika baadhi ya wafanyabiashara wameongeza hata zaidi ya maradufu bei za bidhaa hasa zile za kudumisha usafi kama vile jeli na sabuni maalum.

Akionekana kuwalenga pamoja na supamaketi Rais Kenyatta ameonya kuwa hatua kali kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

“Kwa uhakika si ubinadamu kutumia janga la aina hii kuunda faida kupita kiasi. Tutawachukulia hatua kali watu wanaongeza bei ya bidhaa,” amesema kiongozi huyo wa taifa.

Rais Kenyatta alitoa onyo hilo kwenye mkutano na kikao na wadau wa idara ya fedha wakiongozwa na Gavana wa Benki Kuu Dkt Patrick Njoroge, jijini Nairobi.

Akitoa mfano wa jeli na sabuni, pamoja na vyakula na bidhaa zingine muhimu, Rais amewataka wafanyabiashara kuwa na utu hasa wakati huu janga la Corona linaendelea kuzua taharuki kwa wananchi.

Gavana Njoroge aidha ametoa utaratibu wa kununua bidhaa na kulipia huduma kwa njia ya simu ambapo ada ya malipo yasiyozidi Sh1,000 imeondolewa kwa muda, akisema hatua hiyo itasaidia katika vita dhidi ya ueneaji wa Covid-19.

Dkt Njoroge pia ametangaza kuwa pesa zitakazopelekwa benkini kuanzia sasa zitahifadhiwa kwa muda wa wiki moja, kabla kusambazwa kuendelea kuimarisha uchumi.

Ameelekeza benki na mashirika ya fedha kuwapa muda wa hadi mwaka mmoja wateja waliochukua mikopo kuanzia Machi 2, 2020, ili waweze kulipa bila presha.

Jumatano mchana Kenya imethibitisha visa vitatu vipya vya maambukizi ya Covid-19 na kufanya idadi jumla kuwa wagonjwa saba.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe ameelezea mafanikio kiasi akitangaza kwamba madaktari nchini wamewasiliana kwa video na wale wa China.

Waziri Kagwe hata hivyo amesema visa vya waathiriwa hao ni abiria waliotoka mataifa ya nje.