Habari

COVID-19: Uhuru afungue au asifungue?

July 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

INGAWA wanasayansi wameonya kuhusu hatari ya idadi ya watakaombukizwa virusi vya corona kupanda, Rais Uhuru Kenyatta anawekewa presha afungue nchi ili shughuli za kawaida zirejelewe.

Wataalamu wanasema kuwa vikwazo dhidi ya usafiri havifai kuondolewa wakati huu kwa sababu idadi ya maambukizi inaongezeka badala ya kupungua.

Mnamo Jumamosi Kenya iliandikisha idadi ya juu zaidi ya maambukizi ya watu 389 ndani ya muda wa saa 24, na hivyo kufikisha 7,577 idadi jumla ya maambukizi nchini. Hii ni baada ya sampuli 4,829 kupimwa ndani ya muda huo.

Hii ndio maana Waziri Msaidizi wa Afya Rashid Aman akatoa wito Wakenya kuchukua wajibu wa mtu binafsi wa kuzuia kuenea kwa virusi vya corona kwa kutolegeza kamba katika udumishaji wa masharti yaliyowekwa na wizara hiyo.

“Ningenda kusihi kila mmoja wetu kuchukua wajibu wa kibinafsi kuhusu udhibiti wa ugonjwa huu. Hii ni kwa sababu imebainika kuwa virusi vya corona vinaenea kwa kasi mno katika jamii,” Dkt Aman akasema.

Lakini majuma mawili yaliyopita, Rais Kenyatta alitoa kauli iliyoashiria kuwa huenda serikali yake ikalegeza zaidi vikwazo vilivyowekwa kudhibiti kuenea kwa Covid-19.

“Tutaanza kufungua nchi hatua kwa hatua. Hivi karibuni tutaanza kuruhusu safari za ndege za ndani ya nchi. Sharti maisha yaendelee,” akaambia jopo la washiriki, kwa njia ya video, wakati wa makala ya nane ya mkutano wa shirika la Atlantic Council.

Shirika hili la Amerika hujadili changamoto mbalimbali zinazokumba ulimwengu.

Lakini hivi majuzi Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alikiri kuwa hospitali za humu nchini zimelemewa na ongezo la idadi ya wagonjwa wa Covid-19 kutokana na kuenea maambukizi.

“Hii ndio maana serikali sasa imeanzisha mpango wa kuwatibu na kuwatunza wagonjwa wa corona nyumbani kwa sababu hospitali za serikali hazina nafasi tosha za kuwalaza,” akaeleza.

Ingawa maafisa wa afya bado wanashikilia kuwa kanuni ya kutotangamana, kuvalia barakoa na kunawa mikono kila mara ni muhimu, wanasikitika kuwa watu wengi wamepuuza.

“Siku hizi watu hawakai nyumbani. Watu wamefurika katika barabara za miji huku mikahawa ikiruhusiwa kuendelea na biashara kwa kuzingatia masharti ya idara ya afya ya umma,” akasema Kariuki Njenga.

“Ongezeko la idadi ya maambukizi ni ithibati kuwa watu wetu wanakiuka masharti hayo. Kwa hivyo, hali itakuwa mbaya zaidi ikiwa Rais ataondoa vikwazo vya usafiri kuingia na kuondoka kaunti za Nairobi na Mombasa ambazo zimeandikisha idadi kubwa ya maambukizi,” akasema Dkt Njenga ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza.

Majuma mawili yaliyopita, taifa la Korea Kusini lililolegeza vikwazo mwezi Mei, lililazimika kurejesha marufuku baada ya maambukizi mapya ya Covid-19 kuanza kuchipuza.

Awali, nchi ya Korea Kusini ilisifiwa kwa kufaulu kupunguza kuenea kwa virusi vya corona.

Na juzi, China ililazimika kurejesha amri ya kutotoka nje kwa wakazi 400,000 viungani mwa jiji la Beijing baada ya visa 18 vipya vya maambukizi kuripotiwa.