Habari

COVID-19: Visa 163 vipya, wagonjwa 6 wafariki

December 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

WATU sita wamefariki kutokana na matatizo ya kiafya kwa kuugua Covid-19 katika kipindi ambapo visa vipya 163 vimethibitishwa Jumatatu baada ya sampuli kutoka kwa watu 2,283 kufanyiwa vipimo.

Visa hivyo vipya vilivyotangazwa na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe vinawakilisha kiwango cha maambukizi cha asimilia 7.1 na kufikisha idadi jumla ya maambukizi nchini kuwa 92,055. Na idadi jumla ya waliofariki sasa ni 1,593.

Kwa hivyo, tangu kisa cha kwanza cha ugonjwa huo kigunduliwe nchini mnamo Machi 13, 2020 idadi jumla ya sampuli ambazo zimepimwa ni 973,805.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Waziri Kagwe alisema kuwa Nairobi ingali inaongoza kwa idadi ya maambukizi mapya kwa kuandikisha visa 95. Inafuatwa na kaunti jirani ya Kiambu ambayo iliandikisha maambukizi mapya 15.

Kaunti ya Homa Bay ilikuwa ya tatu kwa kunakili visa vinane, Uasin Gishu (7), Nakuru (6), Machakos (4), Murang’a (3), Kisumu (3), na Trans Nzoia (3).

Nazo kaunti za Mombasa, Kajiado, Meru, Laikipia na Kakamega ziliandikisha visa viwili kila moja huku Isiolo, Makueni,Bungoma, Migori, Nyandarua, Tharaka Nithi, Kirinyaga, Embu, Narok na Vihiga zikiandikisha kisa kimoja kila moja.

Waziri Kagwe pia alitangaza kuwa wagonjwa 424 wamethibitishwa kupona na kuruhusiwa kurejelea maisha ya kawaida ambapo wagonjwa 378 walikuwa wakihudumiwa nyumbani huku wengine wakitibiwa hospitalini.

“Kwa hivyo, kufikia sasa idadi jumla ya wale ambao wamepona ni 73,452 na wale ambao wamelazwa wakipokea matibabu katika hospitali mbali mbali nchini ni 960. Wengine 6,581 wanauguzwa nyumbani,” akasema Bw Kagwe.

Bw Kagwe aliongeza kuwa wagonjwa 49 wako katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICU) huku wengine 27 wakiongezwa hewa ya oksijeni.