Habari

COVID-19: Wabunge watokwa machozi wakisikitikia wahudumu wa afya

November 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

KIOJA kilishuhudiwa katika Kamati ya Bunge kuhusu Afya mnamo Jumatano baada ya wabunge watatu kuangua kilio kutokana na madhila yanayokumba madaktari wakati huu wa janga la corona.

Wabunge James Nyikal (Seme), Sarah Paulata Korere (Laikipia Kaskazini) na Joyce Emanikor (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Turkana) walizidiwa na hisia baada ya kusikiza masaibu ambayo madaktari na wahudumu wengine wa afya hupitia katika vita dhidi ya corona.

Masimulizi hayo yalitolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Nchini (KMPDU) Chibanzi Mwachonda ambaye alisema madaktari wanafariki kwa wingi kwa kukosa bima ya afya, mishahara na marupurupu hitajika licha ya kuhatarisha maisha yao wakiwahudumia wagonjwa wa Covid-19.

Dkt Nyikal alisema alibubujikwa na machozi kutokana na kutelekezwa kwa madaktari na serikali ya kitaifa na zile za kaunti.

“Ningetamani kuwa mkutano huu ungekuwa ukifanyika katika Ikulu na kuongozwa na Rais ili wale ambao humshauri wangesikia,” akasema huku akiangua kilio.

“Hao ndio watu ambao wanapasa kusikiza maelezo haya kutoka kwa madaktari. Ninakerwa mno. Hii sio haki,” akaongeza Dkt Nyikal.

Mbunge huyo wa Seme amewahi kuhudumu kama Mkurugenzi wa Huduma za Afya na Katibu katika Wizara ya Afya wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

Dkt Nyikal pia alilalamikia hali mbaya ya hospitali za umma ambapo wahudumu wa afya wanafanyakazi bila vifaa kinga (PPEs), hali ambayo inahatarisha maisha yao.

Ni wakati huo ambapo wenzake Bi Korere na Emanikor pia walipandwa na hisia na kuanza kububujikwa machozi.

“Kila mtu anasema kuwa madaktari na wahudumu wa afya wanapaswa kuwa wazalendo. Lakini uzalendo haufai kufafanishwa na kujiua,” akasema Dkt Nyikal.

Wabunge hao walikuwa wakitoa kauli zao kutokana na mawasilisho ya Dkt Mwachonda (Katibu Mkuu wa KMPDU) aliyeorodhesha changamoto ambazo madaktari na wahudumu wengine wa afya hupitia.

Chama hicho pia kiliwaambia wabunge kwamba kinataka sekta ya afya isimamiwe na serikali kuu sawa na zile za Usalama na Elimu.

Chama cha KMPDU kimetoa ilani ya mgomo kusukuma serikali kuu na zile za kaunti zishughulikie matakwa yao.

Dkt Mwachonda alisema japo mgomo una madhara makubwa, ni njia ya kipekee ya kuiwezesha serikali kuchukulia malalamishi yao kwa uzito.

“Sitaki kuwa jenerali ambaye anaongoza wanajeshi ambao wanaendelea kuuawa. Sipendi kuwa nikipokea simu kila mara kwamba wenzetu wamefariki kutokana na mambo ambayo tumekuwa tukizungumzia kila mara,” akasema.

Mbunge wa Ndhiwa Mathews Owino ambaye ni mwanachama wa kamati hiyo aliitaka serikali ya kitaifa kuzisambaza PPE zilizoko kwenye maghala ya mamlaka ya Kemsa kwa wahudumu wa afya bila malipo.