Covid-19: Wakenya wamlilia Rais alegeze masharti
Na SAMY WAWERU
Huku Rais Uhuru Kenyatta akitarajiwa kuhutubia taifa leo, Jumamosi, Wakenya wana matumaini makuu kiongozi wa nchi atalegeza kamba kanuni na taratibu zilizowekwa kuzuia usambaaji zaidi wa Covid – 19, ambazo wanataja zimechangia maisha kuwa magumu.
Tangu Kenya iripoti kuwa mwenyeji wa ugonjwa wa Covid – 19, uchumi umezorota kufuatia kuathirika kwa sekta mbambali.
Sekta zinazolia kuathirika kwa kiasi kikuu ni pamoja na biashara, utalii, kilimo, usafiri na uchukuzi, miongoni mwa nyinginezo.
Kafyu ya kitaifa kati ya saa moja jioni na saa kumi na moja asubuhi kila siku pamoja na amri ya kutoingia na kutotoka kaunti zilizotajwa kuathirika kwa msambao wa virusi vya corona, wafanyabiashara wanalalamika kwamba imeathiri biashara zao.
Kutokana na ongezeko la visa vya maambukizi ya corona, Rais Kenyatta aliweka amri ya kutoingia na kutotoka kaunti ya Nairobi, Mombasa, Kilifi na Kwale.
“Tunaomba Rais alegeze masharti ya kafyu, ambayo nusra yafilishe biashara za wengi wetu, wafanyabiashara wa kiwango cha chini na cha kadri (SMEs),” Evelin Irungu ambaye ni muuzaji wa nguo za watoto katika soko la Jubilee, Githurai kiungani mwa jiji la Nairobi ameambia Taifa Leo Dijitali katika mahojiano ya kipekee.
Kulingana na mfanyabiashara huyo ambaye ni mama wa watoto wawili, tangu kisa cha kwanza cha Covid – 19 kiripotiwe Kenya, biashara zimedidimia kutokana na athari za ugonjwa huu ambao sasa ni janga la kimataifa.
Siku zinavyozidi kusonga ndivyo visa vya maambukizi vinazidi kuongezeka, Evelin akisema kiwango cha wateja kinaendelea kushuka ikizingatiwa kuwa watu wanaelekeza mapato yao kwa chakula.
“Kwa mfano, mapato yangu katika biashara ninayatumia kukithi mahitaji ya kimsingi ya familia. Siyarejeshi kuiimarisha. Licha ya kuwa mume wangu anafanya uuzaji wa vitunguu, tunasaidiana katika majukumu, maisha yamekuwa majukumu,” akaeleza mfanyabiashara huyo.
Ikizingatiwa kuwa SMEs inachangia asilimia 50 ya ushuru katika kukuza uchumi, na asilimia 75 ya nguvukazi nchini, sekta hiyo ya juakali imeathirika pakubwa na janga la corona.
Timothy Makutwa, mhudumu wa tuktuk analalamikia kudorora kwa biashara hiyo, hasa amri ya kafyu ilipotangazwa kuanza kutekelezwa mnamo Machi 27, 2020.
Kulingana na mhudumu huyo ambaye awali alikuwa akiingiza zaidi ya Sh2, 000, gharama ya matumizi ikiondolewa, kwa sasa anasema kupata Sh1, 000 ni kwa neema ya Mungu
. “Mbali na kafyu kutuathiri, amri ya kupunguza idadi ya abiria tunaobeba mara moja kwa zaidi ya 60, imefanya mapato yakapungua kwa kiasi kikuu. Jiulize, kubeba abiria wawili kila awamu, kila mmoja akilipa Sh30, Sh1, 000 zitajaa lini?” anashangaa Timothy, ambaye ni baba wa watoto watatu na anayetegemea biashara ya tuktuk kukithi familia yake riziki.
Ombi la mhudumu huyo ni moja tu; “Ndio, tunaelewa ni jukumu letu kama wananchi kushirikiana na serikali na wadau husika kusaidia kuzuia maambukizi, ila tunamuomba Rais Uhuru Kenyatta alegeze masharti ya kafyu.”
Sawa na wafanyabiashara hao, Doreen Kawira, muuzaji wa bidhaa za kula anasema biashara yake inapitia magumu kwa kile anataja kama wakulima kuathirika, hivyo basi mazao kuwa bei ghali. “Kiongozi wa nchi akilegemeza masharti ya uchukuzi, biashara zitaanza kuinuka, hata ingawa itachukua muda,” Doreen anasema.
Erastus Muriuki, ambaye ni mkulima wa nyanya Kirinyaga amesema tangu amri ya kutoingia na kutotoka Nairobi ambako wanatoka wateja wake, imechangia mazao yake kuozea shambani. “Vikwazo vya vizuizi vya maafisa wa polisi barabarani vinalemea wateja wengi kujia mazao shambani,” Muriuki akasema kwenye mahojiano, akihimiza Rais Kenyatta kulegeza masharti ya usafiri.
Juni 1, katika maadhimisho ya sikukuu ya Madaraka Dei 2020, Rais Kenyatta kwenye hotuba yake aliashiria kufungua uchumi mwishoni mwa wiki hii.
Ni suala ambalo linasubiriwa kwa hamu na ghamu leo, Jumamosi, ikizingatiwa kuwa maambukizi ya virusi vya corona nchini yanazidi kuongezeka.