COVID-19: Wizara kutoa mwongozo mpya wa mazishi
Na CHARLES WASONGA
SERIKALI inapanga kuanzisha kanuni mpya ya kuzika watu waliofariki kutokana na Covid-19 baada ya matokeo ya uchunguzi mpya kubaini kuwa virusi vya corona haviwezi kusambaa kutoka kwa maiti.
Akiongea kwenye kikao cha kila siku na wanahabari kutoa taarifa kuhusu hali ya janga hilo nchini, Mkurugenzi wa Afya ya Umma Francis Kuria Jumatatu alisema wizara hiyo itachapisha masharti mapya kuhusu mazishi wiki hii.
Kanuni inayozingatiwa wakati wa mazishi ya watu waliofariki kutokana na corona zimeibia kero kuu watu wakisema haziakisi heshima inayopewa wafu, kulingana na tamaduni za jamii mbalimbali nchini.
Mnamo Aprili 2020 aliyekuwa mfanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA) James Onyango alizikwa usiku nyumbani kwake Ukwala, Siaya na kwa namna isiyoonyesha heshima.
Mwili wake uliletwa na maafisa wa afya waliovalia PPE yakiwemo ‘magwanda meupe’ na walioandamana na maafisa wa usalama.
Isitoshe, alizikwa kwenye kaburi la kina kifupi huku wanajiji wakizuiawa kufika karibu kutoa heshima zao za mwisho, kinyume na taratibu za jamii yake. Ulirushwa ndani ya kaburi hiyo kwa kama mzoga wa mnyama, huku watu wa familia wakilia kwa uchungu.
Kitendo hicho kiliibua malalamishi kutoka kwa viongozi wa eneo hilo wakiongozwa na Seneta James Orengo ambao walisema kinaongeza unyanyapaa kuhusu Covid-19 na hivyo kuhujumu vita dhidi ya janga hilo.
Mnamo Jumatatu, Dkt Kuria alisema kanuni mpya za mazishi zitatoa mwongozo mpya wa unaodumisha hadhi na heshima ya mfu na maafisa wa afya hawatahusishwa pakubwa.
“Baada ya mgonjwa kufariki, hawezi kuambukiza wengine. Usipogusa maji ya mwili huo, uwezekano wa wewe kuambukizwa ni finyu mno. Tunakamilisha masharti mapya yatakayozingatiwa wakati wa mazishi,” Dkt Kuria akasema.
Alielezea matumaini kuwa masharti hayo mapya pia yataondoa unyanyapaa unaohusisha na ugonjwa huo na ambao umewaathiri Wakenya wengi.
“Chini ya masharti hayo mapya hamtawaona watu waliovalia PPE tena katika hafla za mazishi,” Dkt Kuria akaongeza.