COVID-19: Wizara yahimiza Wakenya waendelee kuzingatia masharti
Na SAMMY WAWERU
WIZARA ya Afya ina wasiwasi kuhusu watu kupuuuza sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kuzuia maambukizi ya virusi vya corona kipindi hiki kiwango cha maambukizi kimeonekana kushuka.
Katika muda wa wiki kadhaa zilizopita, maambukizi ya Covid-19 nchini yameonekana kushuka, yakilinganishwa na miezi ya kwanza baada ya kisa cha kwanza kuthibitishwa mnamo Machi 2020.
Wizara ya Afya imesema Jumatano kwamba katika maeneo mengi nchini watu wanaendelea kupuuza sheria na mikakati iliyowekwa, jambo ambalo inahoji ni hatari katika vita dhidi ya corona.
Akitoa taarira ya maambukizi chini ya saa 24 zilizopita, Waziri Msaidizi katika Wizara amesema uchunguzi umeonyesha umma umelegeza kamba suala la uvaliaji maski.
Dkt Aman pia amesema wahudumu wa matatu wanaendelea kukiuka kanuni zilizotolewa, ambapo amataja wanazidi kubeba abiria kupita kiwango kilichopendekezwa na wizara.
Ili kuzuia msambo wa Covid-19 kupitia sekta ya uchukuzi, Wizara ya Afya kwa ushirikiano na ile ya Uchukuzi, ilisema matatu zinapaswa kubeba asilimia 60 ya abiria ya idadi jumla ya kila gari la usafiri. Kwa mfano, matatu ya jumla ya abiria 14, inatakiwa kubeba watu 8 ili kuzuia msongamano wa watu.
Waziri Aman amesema amri hiyo inaendelea kukiukwa, akilalamikia utepetevu huo kutekelezwa maeneo ya mijini na pia mashambani.
Akihutubia wanahabari Afya House, jijini Nairobi, Dkt Aman amesema baadhi ya viongozi na wanasiasa wanaendelea kuandaa mikutano ya hadhara licha ya serikali kuonya dhidi ya mikusanyiko yoyote ile ya umma.
“Timu yetu ya uchunguzi imetembea maeneo mbalimbali nchini na kugundua sheria na mikakati tuliyoweka kusaidia kuzuia maambukizi inanendelea kukiukwa. Changamoto za aina hiyo zinalemaza vita dhidi ya virusi vya corona,” ameonya.
“Ninahimiza umma, hasa katika sekta ya matatu, kwenye masoko na pia wanaoandaa mikusanyiko ya umma, msiturejeshe nyuma katika kampeni kupambana na janga hili,” akasema.
Waziri alisema watu wanavyoidi kukongamana katika maeneo ya umma ndivyo hatari ya kuambukizwa au kuambukiza Covid-19 inaendelea kukolea.
Kufikia Jumatano, Kenya ilikuwa imeandikisha jumla ya visa 35,460 baada ya maambukizi mapya 104 kusajiliwa chini ya saa 24 zilizopita. Waziri alisema asilimia 54 ya visa hivyo ni jinsia ya kiume.