Dalili za moshi mweupe seneti
Na CHARLES WASONGA
HUENDA maseneta wakapitisha mfumo wa ugavi wa fedha baina ya kaunti 47 uliopendekezwa na Kamati ya Seneti kuhusu Fedha na Bajeti, kwenye kikao cha Jumanne wiki ijayo.
Hii ni baada ya uongozi wa seneti kuidhinisha mfumo huo Jumanne kama hatua ya mwisho ya kukomesha mvutano kuhusu suala hili ambalo limechangia serikali za kaunti kukumbwa na changamoto ya kifedha.
“Mfumo uliopendekezwa na Kamati ya Seneti kuhusu Fedha ndio utaidhinishwa ili utumike kugawanya fedha kwa serikali za kaunti,” taarifa fupi kutoka uongozi wa bunge ilisema.
Uongozi wa mrengo wa wengi na ule wa wachache katika seneti unashirikisha wandani wa karibu wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Taarifa hiyo imewasilishwa kwa Afisi wa Spika wa Seneti Kenneth Lusaka na utajadiliwa na kupigiwa kuwa maseneta watakapokutana Jumanne, Septemba 15, 2020.
Hata hivyo, inapendekeza kuwa mfumo utatekelezwe baada ya miaka miwili na kwa awamu ili kuzuia kuvurugwa kwa mipango na bajeti za kaunti mbalimbali.
Mfumo huo umekuwa ukipingwa na maseneta kutoka kaunti 19 zenye idadi ndogo ya watu kwani itapelekea kuaunti hizo kupoteza jumla ya Sh17 bilioni. Kwa upande mwingine kaunti 28 zenye idadi kubwa ya watu zitapokea nyongeza ya mgao.
Chini ya mfumo huo wa kamati hiyo ianyoongozwa na Seneta wa Kirinyaga Charles Kibiru vigezo 10 vitatumiwa katika ugavi wa fedha zitakazotengewa Serikali za Kaunti kutoka Hazina ya Kitaifa.
Asilimia 20 ya fedha hizo zitagawanywa kwa misingi ya hitaji ya huduma za afya, mgao sawa (asilimia 20), idadi ya watu (asilimia 16) na kilimo (asilimia 12), miongoni mwa vigezo vingine.
Kama njia ya kupunguza kiwango cha fedha za ambazo kaunti zitapoteza, taarifa hiyo inasema kuwa ikiwa mfumo huo utapitishwa, hakuna kaunti itapoteza zaidi ya asilimia 10 ya fedha zilizotengewa katika mwaka wa kifedha uliotangulia.
“Kuanzia mwaka wa tatu, kaunti ambazo zitapoteza fedha kupitia matumizi ya mfumo huo mpya zitasaidiwa ili zisiathirike zaidi. Hazitapunguziwa mgao kwa zaidi ya asilimia 10 ya mgao wao wa mwaka wa kifedha wa 2020/2021 ambao ni Sh316.5 bilioni),” uongozi wa seneti unapendekeza kupitia taarifa.
Kimsingi, ikiwa pendekezo hilo litaidhinishwa na maseneta hakuna kaunti ambayo itapoteza fedha au kufaidi zaidi mwaka huu wa kifedha kwani zote zitapokea kiasi cha fedha zilizopokea katika mwaka uliopita wa kifedha wa 2019/2020.
Kamati ya Bw Kibiru inapendekeza kuwa mgao wa mwaka huu uzingatiwa mfumo wa awamu ya pili ambao umekuwa ukizingatiwa tangu 2016 pamoja na matokeo ya sensa ya mwaka wa 2009.
Hazina ya Kitaifa inakadiria kuwa mgao wa fedha kwa kaunti utaongezwa hadi Sh325 bilioni katika mwaka ujao wa kifedha wa 2021/2022 kutoka Sh316.5 bilioni mwaka 2020.
Maseneta wanataka mwaka ujao Sh316.5 bilioni ugawanywe kwa misingi ya mfumo wa awamu ya pili na takwimu za sensa ya 2009 na nyongeza ya Sh9 bilioni zigawanywe kwa misingi ya mfumo mpya wa awamu ya tatu.
Mfumo mpya wa awamu ya tatu utaanza kutumika mnamo mwaka wa kifedha wa 2022/2023. Wakati huo, Hazina ya Kitaifa inakadiria kuwa mgao wa fedha kwa kaunti utakuwa umepanda hadi Sh331 bilioni.
Ni wakati huu ambapo mfumo huu mpya utatumiwa kikamilifu na data kutoka sensa ya mwaka jana, 2019.
Ukadiriaji uliandaliwa na maseneta unaonyesha kuwa, wakati huo, kaunti 16 zitapoteza fedha; hapa ndipo afueni ya asimilia 10 itatumika.
Mnamo Jumanne, Septemba 8, 2020, Spika Lusaka aliahirisha mjadala kuhusu mfumo huo hadi juma lijalo ili kutoa nafasi kwa maafikiano zaidi.
Hii ni baada ya Kamati ya Maridhiano yenye wanachama 12 iliyoteuliwa kusaka mwafaka kuhusu suala hilo kuwasilisha ripoti mbili kinzani. Hii ni ishara kuwa wanachama hawakukubaliana.
Kamati hiyo iliwasilishwa kwa kiongozi wa wengi Samuel Poghisio na mwenzake wa wachache James Orengo. Wenyeviti wenza wa kamati hiyo Moses Wetang’ula na Johnson Sakaja walipendekeza kuwa uongozi wa seneta usake maelewano kwa ripoti moja kati ya hizo mbili.