DCI akamatwa kwa kupoteza bastola yake akibugia pombe kwa baa
AFISA mmoja wa polisi katika Kaunti ya Migori ametiwa mbaroni na wenzake baada ya kupoteza bastola yake alipokuwa akibugia pombe.
Koplo James King’ori wa kitengo cha Ujasusi na Upelelezi wa makosa ya Jinai (DCI) huko Kuria Magharibi, anasemekana kupoteza bastola yake iliyokuwa na risasi 15.
Katika taarifa, afisa huyo anadai kwamba alitembelea baa moja iliyomo mjini Kehancha akiwa ameandamana na rafiki wa kike.
Wawili hao wanasemekana kujitosa katika unywaji wa pombe usiku mzima.
Baada ya kuangusha chupa kadhaa za pombe, afisa huyo anasemekana kusinzia.
Aliamka Jumapili saa kumi asubuhi na kugundua kuwa bunduki yake haipo. Naye mwanamke waliyekuwa naye anasani alikuwa haonekani.
Asijue pa kuanzia na pa kumalizia, alifululiza hadi kituo cha polisi cha Kehancha kuripoti suala hilo.
Mara tu alipomaliza kurekodi taarifa yake, afisa huyo aliwekwa ndani huku uchunguzi wa suala hilo ukianzishwa mara moja.
Kisha mwanamke huyo aliyekuwa akiburudika na afisa huyo alitafutwa na kukamatwa.
Alifungiwa katika kituo hicho hicho.
“Tunatafuta kujua jinsi alivyopoteza bunduki yake. Kwa mfano, tungependa kujua kama mtu alimtilia ‘mchele’ katika kinywaji chake jinsi inavyofanyika katika vilabu vingi vya burudani ili kuwaibia watu mali zao na vitu vyao vya thamani,” alisema afisa mmoja aliyefahamu uchunguzi huo lakini akaomba jina lake libanwe kwa kuwa haruhusiwi kuzungumza na waandishi wa habari.