Habari

DCI lawamani kwa kukosa kukamata wanyakuzi wa ardhi ya Galana Kulalu

Na EDWIN MUTAI July 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

IDARA ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imeelekezewa lawama kwa kufeli kuwatambua watu 10 walionyakua ekari 301,330 ya ardhi ya thamani ya Sh15 bilioni katika renchi ya Galana Kulalu, kaunti ya Kilifi.

Kamati ya Bunge kuhusu Utekelezaji ilisuta kitengo cha kuchunguza ulaghai wa ardhi katika DCI kwa utepetevu baada ya kufeli kuanzisha uchunguzi kuhusu ugavi haramu na unyakuzi wa sehemu ya renchi hiyo inayomilikiwa na Shirika la Ustawi wa Kilimo Nchini (ADC).

Kamati hiyo iliambiwa kuwa DCI haijashughulikia mapendekezo ya Bunge la Kitaifa yaliyopitishwa katika Bunge la 12 yakishauri Tume ya Kupambana na Ufisadi (EACC) kukamilisha uchunguzi kuhusu jaribio la unyakuzi wa ardhi hiyo nambari ADC 1 FR. 119/86 kwa lengo la kuwashtakiwa wahusika.

“Kuhusi ripoti ya Kamati ya Bunge kuhusu Ardhi kuhusu Ombi la Umma Nambari 004 ya 2021 lake Mheshimiwa Michael Kingi, kwa niaba ya wamiliki wa ardhi Magarini, kuhusu kupanuliwa kwa mpaka wa Renchi ya Galana, suala hili halikushughulikiwa na DCI,” George Kisika, aliyetia saini kwa niaba ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai, akasema kwenye barua ya July 21, 2025 na iliyowasilishwa mbele ya Kamati hiyo.

Bw Kisika alifika mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Budalang’i Raphael Wanjala kuelezea kuhusu kiwango cha utekelezaji wa ripoti ya Kamati ya Bunge kuhusu Ardhi kuhusu maombi ya Bw Kingi.

Kamati hiyo ilipendekeza kuwa EACC na DCI zinapasa kukamilisha uchunguzi unaoendelea kuhusu jaribio la unyakazi wa ardhi hiyo ya Renchi ya Galana Kulalu kwa lengo la kuwashtakiwa wahusika.