DCI wateka mazishi ya Gen Z aliyeuawa Saba Saba
MWANAFUNZI wa Kidato cha Tatu aliyepigwa risasi na polisi wakati wa maandamano ya Saba Saba wiki iliyopita alizikwa Jumatano katika hafla iliyotekwa na kusimamiwa na maafisa wa usalama kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI).
Hafla hiyo iligeuka kuwa ya kumtangaza kuwa shujaa, pamoja na vijana wengine waliouawa wakipigania mabadiliko nchini.
Hali ilikuwa ya huzuni, huku hotuba zikikatizwa mara kwa mara na vilio na ghadhabu za waombolezaji. Hii ilichangiwa na hatua ya maafisa wa DCI kuzuia hotuba zozote wakihofia ukosoaji, isipokuwa ile ya kasisi aliyekuwa akiongoza ibada.
Kifo cha James Wambugu, mwana wa afisa wa DCI, pamoja na Julia Wangui, binti wa chifu wa Nturukuma, Martin Kariuki, ni ushahidi tosha kuwa mauaji ya kizazi cha Gen Z yameathiri hata maafisa wa serikali, na lawama kuelekezwa kwa utawala wa Kenya Kwanza chini ya Rais William Ruto.
Mapema Jumatano saa kumi na mbili alfajiri, maafisa wa DCI walifika katika mochari ya Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Nanyuki na kuchukua mwili wa Wambugu, mwenye umri wa miaka 23, kisha wakasindikiza jeneza hadi nyumbani kwa wazazi wake kijijini Katheri, takriban kilomita nane kutoka mjini.
Hatua hiyo, ambayo iliwashangaza jamaa wa familia, ilichochewa na taarifa kuwa vijana walikuwa wamepanga kuliteka jeneza na kulipeleka katika kituo cha polisi cha Nanyuki.
“Tuliagizwa usiku kuwa tufike mochari saa kumi na mbili alfajiri. Na kweli, maafisa wa DCI walikuwepo kusindikiza jeneza hadi nyumbani,” alisema mmoja wa jamaa wa familia ambaye hakutaka kutajwa.
Na msafara ulipowasili nyumbani saa moja asubuhi, maafisa wa DCI walichukua usukani wa ratiba na kumwamuru MC Bw David Murithi kuruhusu familia ya karibu pekee kuzungumza, huku wakisisitiza wasizungumzie masuala tata.
“Mtaniwia radhi kwa kuzuia baadhi ya watu kuzungumza, lakini nimepewa maagizo madhubuti kupunguza idadi ya wazungumzaji. Najua kuna wanaowania nyadhifa mbalimbali za kisiasa, lakini watuvumilie,” alisema Bw Murithi.
Hata hivyo, Kasisi Roy Mwiti aliyeongoza ibada alikataa kunyamazishwa, akifichua kuwa kulikuwa na juhudi za kuingilia hotuba yake. Alitoa mahubiri makali yaliyoikosoa vikali serikali ya Kenya Kwanza.
“Kwa maafisa wa polisi na taasisi nyingine za serikali zinazohusika katika kuwaua vijana wanaotoa malalamishi yao halali, mwaweza kuua miili yao, lakini hamtaweza kuzima roho zao. James aliuawa kishujaa kwa kupigwa risasi na polisi. Ingawa tumemzika leo, roho yake itaendelea kuishi,” alisema kasisi huyo wa Parokia ya Katheri/Ndemu.
Katika mahubiri yake, kasisi huyo aliwaonya polisi wanaotekeleza maagizo ya wakubwa wao kwa upofu kuwa vitendo hivyo vitawatesa maisha yao yote. Alisema kuwaua waandamanaji wakiwa na amani waliokuwa na bendera ya taifa, chupa za maji na simu ni unyama wa hali ya juu.
“Mnaweza kuua mkilinda kazi zenu, lakini hata mkijikusanyia mali kupitia vitendo vya kishetani, hamtajua amani. Huenda hatujui ni nani aliyempiga risasi mwanafunzi huyu, lakini popote alipo, sina shaka hana usingizi wa amani,” alisema Kasisi Mwiti.
Viongozi wa eneo hilo waliodinda kukemea mauaji ya vijana mikononi mwa serikali pia walikosolewa vikali na kasisi huyo pamoja na wazungumzaji wachache waliopambana hadi wakaingia jukwaani.
Bi Joyce Wangui, mtetezi wa haki za binadamu, aliyeruhusiwa kuhutubia waombolezaji na kasisi, aliwalaumu viongozi waliochaguliwa kwa kushindwa kukemea polisi kuhusu mauaji ya vijana.
“Polisi wameagizwa kuwapiga risasi waandamanaji risasi kwenye miguu. Wapo waliopigwa mguuni na bado wakafariki. Waendelee kuua, lakini siku yao ya hukumu inakuja, tutakapoiondoa serikali hii kwa kura,” alisema Bi Wangui.
Wambugu alikuwa kitinda mimba wa afisa wa DCI, Bw Lawrence Kiriinya, na alipigwa risasi katika mtaa wa Likii, Nanyuki, mnamo Julai 7, 2025.
Ripoti ya upasuaji wa mwili uliofanywa Jumanne mbele ya mashirika kama Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (KNCHR), Chama cha Wanasheria (LSK), Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) na mashirika mengine ya haki, ilionyesha kuwa alifariki kutokana na kuvuja damu kwa wingi baada ya kupigwa risasi.