DeMathew atajwa kama Nabii wa Mlima Kenya
NDUNGU GACHANE NA CHARLES WASONGA
VIONGOZI na mashabiki wa marehemu John DeMathew wamepokea habari za kifo chake kwa mshangao huku wanamuziki wenzake wakijawa na huzuni kuu kwa kumpoteza mwenzao.
DeMathew ambaye amedumu katika ulimwengu wa muziki kwa miaka 54 alifariki Jumapili usiku baada ya gari lake kugongana na trela ndogo katika barabara kuu ya Thika, karibu na mkahawa wa Blue Post.
Alipata majeraha kichwani, miguuni na kifuani na akafariki alipofikishwa katika hospitali ya Thika Nursing Home, mjini Thika.
Kufuatia kifo cha DeMathew viongozi wa Murang’a wakiongozwa na Gavana Mwangi Wa Iria walimwomboleza na kumtaja kama Nabii wa jami ya Agikuyu na msanii mwenye talanta ya kipekee.
Walisema marehemu alitumia muziki kama chombo cha kuonya, kufundisha, kuburudisha na kuzindua jamii ya Agikuyu kuhusu masuala mbalimbali katika ulimwengu wa siasa, mahaba, mihadarati na pombe haramu.
Kwenye risala yake ya rambi rambi, Gavana Wa Iria alisema serikali itashirikiana na familia na marafiki wa DeMathew kuandaa mazishi yake.
“Vile vile, natoa wito kwa wanamuziki kuendelea kuchangia Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo (Sacco) cha Talented Musicians and Composers Sacco (Tamco) ambacho marehemu alihudumia kama mwenyekiti,” akaongeza.
Bw Wa Iria akaongeza: “Jamii ya Agikuyu imepoteza msanii aliyeiongoza, kuilekeza na kuishauri kuhusu masuala mbalimbali. Na alidhihirisha sifa za uongozi kwa kuwa mwenyekiti wa chama cha Tamco Sacco kilichoanzishwa mapema mwaka huu.”
Aliwashauri wanamuziki kuendelea kukipiga jeki chama hicho cha ushirika ili kustawi na kuweza kuwasaidia wanamuziki wengi wa sasa na wanaoibuka.
Mbunge wa Gatundu Kaskazini Moses Kuria alisema amepokea habari za kifo cha DeMathew kwa huzuni akimtaja kama rafiki wake mkubwa.
“Nimepokea habari za kifo hichi kwa mshangao na huzuni kuu. Marehemu alikuwa rafiki, ndugu na mshauri wangu mkubwa kuhusu masuala ya kijamii na kisiasa. John hakuwa masanii wa kawaida; alikuwa Nabii wa jamii ya Agikuyu sawa na wanamuziki wa zamani marehemu Joseph Kamari na Muigai wa Njoroge” akaeleza Bw Kuria.
Mbunge wa Gatanga Nduati Ngugi, ambako marehemu DeMathew anatoka, naye alisema eneo bunge lake lipata pigo kubwa zaidi kufuatia kifo hicho.
“DeMathew aliweka eneo bunge letu katika ramani ya ulimwengu kutokana umaarufu wake katika ulimwengu wa muziki. Alikuwa miongoni mwa mwanamuziki wa jamii ya Agikuyu ambao walitoa mwelekeo wa kisiasa na kijamii kwetu. Ni huzuni kuu kwamba tumempoteza kupitia ajali ya barabarani,” akasema.
Baadhi ya tungo za marehemu ambazo zilivuma ni kama vile “Njata yakwa” “Kireke tuturainie”, “Arume kwi nambu”, “Nengereria kane”, “Meme mene Tekeli”, “Mwihuguro”, “Pin Number”, Kireke tuturanie” miongoni mwa vibao vingine vyenye maudhui mazito.
Katika albanu yake “Njata yakwa” marehemu DeMathew anamshirikisha Mbunge Mwakilishi wa Murang’a Sabina Wanjiru Chege katika wimbo huo wa mahaba na uliosanifishwa kwa muundo wa ushairi.
Kabla ya kifo chake Jumapili, marehemu alikuwa amehudhuria mchango wa fedha mjini Thika kwa ajili ya kukusaidia mwanawe mwanamuziki Peter Kigia ambaye mwanawe anaugua.
Mwanamuziki Apha Maina aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba walishinda na DeMathew kwa saa nyingi Jumapili katika harambee hiyo.
Maina alisema baada ya harambee hiyo, DeMathew aliombwa atie saini stakabadhi fulani kwa ajili ya ujenzi wa jengo katika kipande cha ardhi walichonunua juzi katika eneo la Kenol lakini hakufanya hivyo.
“Badala yake aliitisha mkutano mnamo Jumanne kwa sababu saa zilikuwa zimesonga zaidi. Kwa hivyo sikuamini nilipopata habari kuhusu kifo chake” Bw Maina, ambaye mmoja wa maafisa wa Tamco Sacco, aliambia Taifa Leo.
Chama hicho kilikuwa kimenunue kipande cha ardhi mjini Kenol ambako kilipanga kujenga studio za kurekodi muziki na kituo cha kukuza talanta za muziki.
Wanamuziki walibuni wazo la kubuni Sacco baada ya kifo cha Joseph Kamaru ambapo iliwalazimu kuchanga fedha za kufadhili mazishi yake kwani familia yake haikuwa na uwezo wa kumuda gharama hiyo.
“Kamwe hatutafanya mchango tena kugharamia mazishi ya mmoja wetu au kuomba fedha za kulipia bili za matibabu,” DeMathew akanukuliwa akisema wakati huo mwaka jana.