Dhehebu la 'Nabii' Owuor lilivyotumia 'injili' kunyakua mali ya muumini
Na AGEWA MAGUT
DHEHEBU linaloongozwa na David Owuor la Ministry of Holiness and Repentance, Jumapili lilijipata motoni wakati familia moja ya Nairobi ilipodai limempumbaza jamaa wao, kwa nia ya kumpokonya mali.
Mvutano ulitokea nyumbani kwa mwanamke huyo, wakati jamaa zake walipozozana na wawakilishi wa kundi hilo la kidini, wakidai wananyakua mali ya mpendwa wao.
Jamaa hao walidai dada yao, Bi Jane Njagi, ambaye ni wakili aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni ya J. M. Njagi Advocates, alipumbazwa kwa “mahubiri ya kupotosha” katika kanisa la Kings Outreach, lililo chini ya Owuor.
Kulingana na familia hiyo, wasimamizi wa kanisa hilo “walimhadaa” dada yao asalimishe mali yake ikiwemo nyumba ya kifahari na magari ya bei ghali, “ili zitumiwe na kanisa”.
Walisema imekuwa vigumu kwao hata kuwasiliana na dada yao bila kupitia kwa msaidizi wake, ambaye pia ni muumini wa dhehebu hilo.
Walinzi katika lango la nyumba ya Bi Njagi, iliyo katika barabara ya Rapta mtaani Westlands, walikataza familia yake kuingia wakidai alikuwa amelala.
Dadake, Bi Alice Macharia, aliambia wanahabari kuwa Bi Njagi amepewa ulinzi mkali, kiwango cha kufanya iwe vigumu hata kufahamishwa kwamba mamake alifariki.
Ilibidi kaka yao aliyetambuliwa kama Duncan, aende na tangazo la kifo cha mama yao lililochapishwa gazetini, ndipo akaruhusiwa kumfikishia ujumbe huo.
Mwakilishi wa kanisa la Kings Outreach, ambaye pia ni wakili, Bw Kimani Watenga, alithibitisha mwanamke Bi Njagi ni mshirika wa dhehebu lao.
Alisema Bi Njagi ni askofu katika dhehebu hilo na “alistaafu” kutoka kazi yake ya uwakili, ili atumie muda wake kutumikia kundi hilo.
Bw Kimani alidai kwamba kupitia maombi, mwanawe Bi Njagi aliponywa ugonjwa wa kushindwa kusoma (dyslexia).
“Kama njia ya kutoa shukrani kwa muujiza huo, Bi Njagi alikabidhi nyumba yake mtaa wa Riverside Drive kwa dhehebu ili itumiwe kwa mafunzo ya Biblia,” akasema Bw Kimani.
Lakini familia ya Bi Njagi ilidai kanisa lilichukua nyumba hiyo na kuigeuza kuwa afisi zake kuu.
Kwa upande wake, Bw Kimani alitetea kundi lao na kusema hawana haja ya kunyakua mali ya Bi Njagi na akitaka wahame watafanya hivyo.
Ilisemekana kwa sasa Bi Njagi anaishi na mwanamke anayefahamika kama Bi Lily Muthoni Macharia, ambaye ni muumini wa dhehebu hilo.
Familia ilidai kuwa Bi Muthoni aliajiriwa kusimamia mali ya dada yao, lakini Bi Muthoni akajitetea kuwa aliona Bi Njagi husahau mambo haraka, ndiposa akaamua kumsaidia kwa hiari kusimamia fedha zake ili asitapeliwe.
Hivi majuzi, dhehebu la Owuor, ambaye wafuasi wake humtambua kama ‘nabii’, liligonga vichwa vya habari wakati ilipodaiwa mwalimu ambaye ni mfuasi wake aliteka nyara mwanafunzi Muislamu jijini Nairobi, kwa lengo lka kumgeuza imani awe Mkristo.
Familia ya msichana huyo ilimshtaki mwalimu husika, Bi Evelyn Awuor Omolo kwa utekaji nyara na akaachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000.
Mwishoni mwa mwaka uliopita, maafisa kadhaa wa polisi walijikuta matatani wakati Inspekta Jenerali wa Polisi, Bw Joseph Boinnet alipoagiza wachunguzwe kwa kumpa Owuor ulinzi mkubwa kupita kiasi alipokuwa Nakuru.
Wafuasi wake wanamchukulia kama mjumbe aliyetumwa na Mungu kuokoa wanadamu, na anapozuru mji huwa wanaosha barabara anakopitia kwa maji na sabuni.