DIGRII ZA MAJUTO: Vibarua licha ya kusoma
Na BENSON MATHEKA
UKOSEFU wa kazi nchini umefikia kiwango cha kutisha na kulazimu vijana wengi wanaofuzu katika vyuo vikuu kufanya kazi za mikono zisizohitaji masomo.
Baadhi yao wanalazimika kufanya kazi za sulubu zikiwemo kusukuma mikokoteni, uchuuzi na vibarua vya mijengo.
Wengi wao waliohojiwa na Taifa Leo wanajuta kwa nini walitia bidii kwa miaka 16 shuleni ili kupata digrii, na baadaye wakajipata wanafanya kazi ambazo hazihitaji hata mtu kuingia Darasa la Kwanza.
Mmoja wao ni Kennedy Sangoey, ambaye alihitimu 2011 na shahada ya uhandisi kutoka Chuo Kikuu cha Egerton, na kwa sasa anafanya kazi ya mjengo kujikimu.
Anasema baada ya kukosa kazi alihisi hakuwa na elimu ya kutosha na akatafuta ufadhili wa kuongeza masomo katika chuo kikuu kimoja nchini China lakini bado hajafaulu kuajiriwa.
“Nina mrundiko wa vyeti lakini sijafaulu kupata kazi. Inatamausha kuwa baada ya kusoma chuo kikuu na kufuzu kuwa mhandisi mimi na familia yangu hatujaona matunda ya elimu. Kijijini watu huniita mhandisi lakini hawaoni huyo mhandisi. Mimi ni mhandisi kwa jina tu!” asema.
Sangoey hulipwa Sh600 kwa siku katika kazi ya mjengo: “Sio kazi ninayofurahia kufanya lakini kwa sababu nina mahitaji lazima niifanye,” aeleza.
Kijana huyu asema kukosa kazi kumezima ndoto yake ya kuhakikisha mama yake mzazi anaishi maisha mazuri baada ya kuteseka akimsomesha na anajuta kwa nini alichagua kusomea uhandisi.
“Huwa ninajuta na kufikiri kama ningesomea uanasheria au udaktari labda maisha yangekuwa tofauti kwa sababu sekta hizo zinaonekana kuwa na nafasi zaidi za ajira,” adokeza.
Naye Samuel Gachini, ambaye ni mkazi wa Thika aliyefuzu kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta 2012 na kusomea uzamili katika Chuo Kikuu cha Moi, asema ukosefu wa kazi umemsukuma kufanya kazi ya teksi.
Bw Gachini ameamua kuongeza masomo na sasa anasomea uzamifu (PhD). “Wakati mwingine huwa ninahisi kuvichoma vyeti vyangu kwa sababu havinisaidii. Muda unasonga na ndivyo watu wanaendelea kufuzu na kupunguza nafasi ya waliotangulia kupata kazi,” asema Bw Gachini.
Kwa miaka minne sasa amekuwa akiendesha teksi ili apate pesa za kujikimu kimaisha.
“Mtu hutamauka anapofikiria muda na nguvu alizowekeza kupata elimu ya chuo kikuu. Watu huwa wanashangaa wakiona ukifanya kazi ya kuendesha teksi ilhali una digrii.”
“Watoto huwa wanaangalia picha za wazazi wao walipokuwa wakifuzu lakini wale wa majirani wanawaambia baba yako ni dereva wa teksi. Inauma sana!” asema na kuongeza kuwa ana matumaini siku moja atapata kazi afurahie matunda ya bidii yake masomoni.
Kwa upande wake, Isaac Cheruiyot, 25, anajuta kwa nini alijiunga na chuo kikuu kwani ametafuta kazi kwa miaka minne bila mafanikio baada ya kufuzu vyema na digrii ya masuala ya utafiti.
“Huwa ninajuta na kusema heri ningepatiwa pesa nilizolipiwa karo kuanzisha mradi wa kuniletea mapato,” asema.
Anasema alipofuzu kutoka Chuo Kikuu cha Karatina mnamo 2017, alitarajia digrii yake ilikuwa tiketi ya kupata kazi inayolingana na taaluma yake.
KUFUZU KUPINDUKIA
“Nilipofuzu katika sayansi ya utafiti wa maikrobaiyolojia, nilidhani nilikuwa na tiketi ya kufanya kazi katika ofisi kubwa lakini ilikuwa ndoto tu,” asema kijana huyu ambaye amegeukia ufugaji.
“Sifurahii ninachofanya. Nifanya hivi kujikimu tu. Nilitia bidii masomoni. Ndoto yangu ilikuwa niwe mwanasayansi mtajika. Watu wanaponiona nikichukua jembe kuingia shambani wanacheka kwa sababu wanasema nilitumia miaka minne chuo kikuu na sina tofauti wale hawakusoma,” anasikitika.
Kijana huyu ana machungu akikumbuka siku moja ambapo alinyimwa kazi kwa sababu ya kuwa na digrii.
“Mnamo 2019 walitangaza kazi za muda katika serikali. Nilituma ombi na nikaitwa kwa mahojiano lakini walipoangalia vyeti vyangu waliniambia sifai kufanya kazi hapo. Nilipowauliza sababu waliniambia mimi ni mwerevu sana. Nilivunjika moyo kwa sababu ukijua uko na uwezo wa kufanya kitu na unyimwe nafasi ya kukifanya unakasirika,” alisema.
Valentine Ochieng, 29, ayefuzu na shahada ya masuala ya safari za ndege kutoka Chuo Kikuu cha Moi mnamo 2016 lakini sasa ni mchuuzi wa samosa katika mitaa ya jiji la Nairobi baada ya kukosa kazi.
“Nimetuma maombi ya kazi katika kampuni nyingi za safari za ndege na sijafanikiwa. Niliamua kutafuta mbinu za kujikimu kwa kuwa mchuuzi,” asema.
Kabla ya kuanza kuuza samosa, Bi Ochieng alikuwa akichuuza matunda.