Diwani asaka haki mwaka moja baada ya mwanawe wa pekee kuuawa
DIWANI maalum wa Kaunti ya Kirinyaga, Lucy Njeri, 45, anakabiliana na majonzi, kusaka haki na matumaini ya mwanzo mpya kufuatia mauaji ya binti yake wa pekee, Seth Nyakio, mnamo Oktoba 14, 2024.
Nyakio, 23, mahafala wa Taaluma ya Mawasiliano ya Vyombo vya Habari kutoka chuo kikuu cha kibinafsi mjini Thika, aliuawa katika nyumba ya kukodisha katika makazi ya Biafra Estate.
“Ulikuwa wakati wenye uchungu zaidi maishani mwangu. Tulikuwa na uhusiano wa karibu mno, wandani…Kisha, akiwa na umri wa miaka 23, aliuawa,” alisema Bi Njeri.
Siku ya mkasa huo, Bi Nyakio aliondoka nyumbani kwao Kamakis Estate, Kiambu, kumtembelea rafiki.
Rafiki yake, Phoebe Mwende, aliripoti kumwacha akiwa amelala asubuhi kabla ya kupata ameaga dunia aliporejea adhuhuri.
Ripoti ya upasuaji ilifichua alinyongwa kwa mikono huku akifunikwa pua na mdomo.
Mshukiwa mkuu, Ken Kimanthi, almaarufu Sultan, 27, mwanafunzi katika Chuo cha Ufundi cha Thika, alikwepa kukamatwa kwa zaidi ya mwaka mmoja akihamia kaunti za Kiambu, Nairobi, Meru, Tharaka Nithi, Nakuru na Busia.
Alikamatwa hatimaye mjini Busia karibu na mpaka wa Kenya–Uganda, alipokuwa akifanya kazi katika duka la kuuza nafaka.
Bi Njeri anasema kukamatwa kwa mshukiwa na kufikishwa katika mahakama ya Kahawa, Desemba 15, 2025, kuliashiria mwanzo wa kukabiliana na simanzi yake.
“Najua siwezi kuomboleza milele. Nitalazimika kuishi na uhalisia wa kupoteza na kutafuta namna ya kufarijika,” alisema Diwani huyo akiorodhesha mpango wake – kufuatilia kesi hiyo, kutafuta uwezekano wa kuwa mama, kupona na kusonga mbele.
Angali na matumaini ya kumpa Nyakio mdogo wake, akisema, “natafakari kuhusu furaha ambayo angehisi Nyakio akiwa mbinguni kuniona nikimpakata mdogo wake. Mwenyezi Mungu atatuliza dhoruba iliyomo maishani mwangu. Nitashinda kwa sababu Mungu wangu anaishi.”