Habari

DONDOO: Pwagu apata pwaguzi polo akiachia demu bili ya deti Ruiru

Na SAMUEL MUIGAI March 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

DEMU alijipata pabaya baada ya polo waliyekuwa naye katika deti kuhepa na kumuachia bili kubwa, eneo la Kamakis, Bypass ya Ruiru jijini Nairobi.

Wawili hao walipatana kwa mitandao na wakaanza kurushiana mistari kishakani.

Muda si muda walipanga siku ya kukutana ili wafahamiane uso kwa uso na kujivinjari.

Siku ya kisa wote walitokea kama walivyoagana kisha wakafululiza hadi kilabu moja kupata vinywaji.

Polo alishangaa kuona kidosho akiitisha vinywaji vya bei kali, moja baada ya nyingine.

Isitoshe, simu yake ilikuwa inapigwa kila baada ya muda na alikuwa akisonga kando kuipokea.

Jamaa akajifanya hamnazo kumbe amechomoza masikio kusikia kwa makini kinachosemwa, na hapo aligundua kumbe mwanadada alikuwa akipanga deti nyingine sehemu tofauti wakishaagana.

Papo hapo, boychild akaanza kusuka mbinu ya kutoroka. Nafasi ilitokea wakati simu ya demu ilipigwa tena. Aliipokea na kusonga mbali kama kawaida ili jamaa asipate mawasiliano yake.

Kumbe pwagu kapata pwaguzi; jamaa alijinyanyua pole pole kitini kana kwamba anaenda msalani, akapenya kwa mlango wa nyuma na kuingia mitini.

Kipusa alipomalizana na maongeo ya simu alirudi mezani lakini hakumpata polo. Nusra azirai alipompigia simu na kupata jamaa ni mteja.

Ilibidi mwanadada abembeleze marafiki zake wamtumie senti kwenye Mpesa alipe bili ya vinywaji aliyoachiwa la sivyo angelazimika kupiga deki kilabu kizima.