DPP azimwa kumshtaki Mbunge Jayne Kihara kwa uchochezi
MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga amezimwa na mahakama kuu kuendelea na kesi ya uchochezi dhidi ya Mbunge wa Naivasha Jayne Wanjiru Kihara.
Akimkanyagia DPP breki, Jaji Chacha Mwita alisema kesi aliyowasilisha Kihara imezua masuala chungu nzima ya ukiukaji wa haki zake za uhuru wa kusema na mawasiliano kwa ujumla.
Jaji Mwita alimwagiza DPP asiendelee na kesi aliyomfungulia Kihara akidai aliwachochea wakazi wa eneo analowakilisha bungeni la Naivasha kwa kuwapa vidokezo kuhusu uhalifu uliotokea wakati wa maandamano ya Gen Z Juni 25, 2025.
Katika shtaka lililowasilishwa mbele ya hakimu mwandamizi Benmark Ekhubi, mahakama ya Milimani Nairobi, DPP alisema matamshi ya Kihara kuhusu maandamano hayo yaliyokumba kaunti nyingi nchini yalilenga kuhatarisha amani.
Kupitia kwa wakili mwenye tajriba ya juu (SC) Kalonzo Musyoka pamoja na mawakili C N Kihara na Njiru Ndegwa, Kihara aliwasilisha kesi mahakama kuu akiomba kesi aliyoshtakiwa na DPP ifutiliwe mbali kwa vile inakandamiza haki zake kama Mbunge wa eneo la Naivasha.
Mawakili hao walihoji uhalali wa kesi hiyo wakisema haki za kuzugumza ambazo kila Mkenya yuko huru kujieleza na kutoa maoni kwa mujibu wa kipengee nambari 33 cha Katiba.
“Kama mtunga sheria Kihara anapasa kuwaeleza watu anaowakilisha bungeni athari za sheria hizo na faida zake,” wakili Kihara alimweleza Jaji Mwita.
Mawakili wameeleza mahakama kuu sheria nambari 94 anayodaiwa aliivunja inapasa tu kushtakiwa walevi.
Akisitisha kwa muda kushtakiwa kwa Kihara, Jaji Mwita alisema kesi aliyomshtaki Mwanasheria Mkuu, Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen yahitaji kuamuliwa ndipo korti itathmini uhalali wa kesi ya uchochezi aliyoshtakiwa Kihara.
Jaji Mwita aliwaamuru washtakiwa wajibu kesi dhidi yao katika muda wa siku saba na kuorodhesha kusikizwa kwa kesi hiyo Septemba 16, 2025.
Kihara alikataa kujibu shtaka aliloshtakiwa na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000.