Habari

DStv kufukuzwa Ghana isipopunguza ada ya huduma

Na REUTERS August 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ACCRA, GHANA

SERIKALI ya Ghana imeipa Kampuni ya Matangazo kupitia Mawimbi ya Satelaiti, DStv makataa ya hadi Alhamisi kupunguza ada zake la sivyo leseni yake ifutwe.

Waziri wa Mawasiliano Samuel Nartey George alisema kuwa aliamrisha Mamlaka ya Kitaifa ya Mawasiliano (NCA) ianze mchakato wa kuondoa leseni ya MultiChoice Ghana ambayo hupeperusha matangazo chini ya DStv iwapo itakosa kupunguza bei kufikia Agosti 7.

“Nimeamrisha NCA ichukue hatua za haraka ili kufikia Agosti 7 iwapo DStv haitakuwa imepunguza bei yake, leseni yao iondolewe mara moja,” akasema George.

Utata huo ulizuka baada ya DStv kupinga pendekezo la serikali kuwa ipunguze bei yake kwa asilimia 30. George alishutumu usimamizi wa DStv kwa kuendelea kutoza bei ya juu wakati ambapo uchumi wa Ghana nao unaendelea kutikiswa na changamoto mbalimbali kwa sasa.

“Uaminifu wangu ni kwa raia wa Ghana ambao wamedanganywa kwa miaka mingi na ni wakati wa kumaliza ukora huo,” akaongea.

MultiChoice Ghana, nayo imepinga shinikizo za kuitaka kupunguza bei, ikisema kuwa itasababisha ajira kupotea na kuvuruga ubora wa huduma zake hasa wakati huu wa uchumi mgumu.

“Ajira zitapotea na tumewasilisha mapendekezo mengine kwa serikali kutatua utata huu,” akasema Mkurugenzi Mkuu Alex Okyere.

George kupitia X hata hivyo alipinga mapendekezo hayo akisema hayana mashiko.

Alihoji kwa nini MultiChoice ilitii amri ya kortini na kupunguza bei kwa wateja wake Nigeria wala si Ghana.