Duale akanusha wasimamizi wa SHA huajiriwa kwa upendeleo wa kikabila
Bw Duale aliambia wabunge Naivasha uajiri wa wafanyakazi wa SHA ulizingatia kikamilifu misingi ya uwezo na sifa.
Wakati huo huo, Waziri wa Elimu, Bw Julius Ogamba, alijikuta kona mbaya mbele ya Wabunge alipokuwa akijibu maswali kuhusu hali ya elimu nchini.
Bw Ogamba aliwashangaza wabunge alipofichua kuwa Wizara ya Elimu haina takwimu kamili za gharama halisi ya kumsomesha mtoto kuanzia Gredi ya Kwanza hadi chuo kikuu.
“Kwa hakika, kama nchi, hatujui ni kiasi gani kinahitajika kumsomesha mtoto kuanzia Gredi ya Kwanza hadi chuo kikuu,” Bw Ogamba aliwaambia wabunge wakati wa kikao kinachoendelea Naivasha, Kaunti ya Nakuru.
“Kwa mfano, serikali hutoa mgao wa Sh1,420 kwa elimu ya msingi bila malipo, Sh15,000 kwa shule ya Sekondari msingi, na Sh22,000 kwa Sekondari Pevu. Pia kuna mchango wa Hazina ya Serikali ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF), kaunti hutoa basari, michango ya harambee na kuna ufadhili wa sekta ya kibinafsi,” alisema.
Bw Ogamba alisema hakuna utafiti wa kitaalamu ambao umefanywa kubaini gharama halisi ya elimu ya mtoto kuanzia chekechea
hadi chuo kikuu.
Aliwaambia wabunge waliokuwa na hasira kuwa Wizara ya Elimu, kupitia mabadiliko yanayoendelea ya mfumo wa kusimamia habari za elimu Kenya (Kemis), inaandaa mfumo utakaompa kila mwanafunzi nambari ya kipekee kuanzia ECDE hadi chuo kikuu.
“Hii itatuwezesha kupata kiwango halisi cha gharama ya kumsomesha mtoto hadi chuo kikuu. Mfumo huu pia utatusaidia kubaini iwapo tukiweka fedha zote pamoja, tunaweza kutimiza masharti ya Kifungu cha 53 cha Katiba kuhusu elimu bila malipo na ya lazima,” alisema.
“Tunahitaji kukabili suala hili moja kwa moja ili kupata taswira kamili ya kiasi cha fedha kinachopaswa kutengewa kila mwanafunzi.”
Masuala ya uteuzi wa wanafunzi wa Gredi 10, mpito kutoka Sekondari Msingi, ufadhili wa shule na tofauti za miundombinu yalitawala kikao hicho huku wabunge wakimiminia Waziri maswali mazito wakitaka majibu ya wazi.