Habari

Dunia yapumua

November 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

VALENTINE OBARA na MASHIRIKA

ILIKUWA ni furaha ulimwenguni kote mashirika ya habari Amerika yalipotangaza kuwa Joe Biden ametwaa urais wa nchi hiyo na kumwangusha Rais mbishani Donald Trump.

Tangu aingie mamlakani miaka minne iliyopita, Trump, 74, alichochea hamaki miongoni mwa raia wengi wa Amerika na ulimwenguni kote kwa jumla.

Hii ni kutokana na maamuzi mengi aliyoyafanya yaliyolenga kukandamiza uhuru na haki, hasa kwa watu weusi na raia wasio ‘Waamerika halisi’.

Jumamosi, mashirika ya habari yaliripoti kuwa Biden, 77, ndiye sasa ataapishwa kuwa rais wa 46 wa nchi hiyo iliyo na ushawishi mkubwa ulimwenguni.

“Amerika, nimefurahi kuwa mmenichagua kuongoza nchi yetu tukufu. Kazi inayotusubiri si rahisi, lakini nawaahidi hili: Nitakuwa rais wa Waamerika wote – uwe ulinipigia kura au la. Nitadumisha imani mlioniwekea,” akasema Biden katika taarifa punde baada ya matokeo hayo kutangazwa.

Lakini Trump hakupoteza muda, akasisitiza yeye ndiye mshindi halisi wa uchaguzi huo ambao umegawanya Waamerika sana kiasi cha kusababisha maandamano na ghasia ambazo si kawaida wakati wa uchaguzi nchini humo.

“Sote tunajua kwa nini Joe Biden anaharakisha kujitangaza mshindi kwa udanganyifu, na kwa nini marafiki wake katika mashirika ya habari wanajaribu sana kumsaidia. Hawataki ukweli ujulikane. Ukweli uliopo ni kuwa uchaguzi haujakamilika,” akasema Trump.

Alipoingia mamlakani mnamo 2016, hakupoteza muda bali alianza kusimamia upitishaji wa sera na sheria ambazo zililenga kuwafungia nje raia wa nchi za kigeni.

Sheria ilipitishwa kuzuia raia wa nchi kadha za nje ambazo alidai zina magaidi wengi wasiingie Amerika.

Kando na hayo, utawala wake ulifadhili ujenzi wa ukuta katika mpaka wa Amerika na Mexico, akidai lengo lilikuwa kuwafungia nje walanguzi wa mihadarati na wahalifu wengine.

Mienendo hii iliwatia nguvu Waamerika wanaodharau watu weusi, kiasi cha kwamba ripoti zinasema mauaji ya watu weusi yaliongezeka katika kipindi cha utawala wake.

Mauaji hayo inaaminika yalirahisishwa na sheria alizofadhili zilizowezesha raia kumiliki bunduki kwa urahisi mno.

Ni hali hii iliyosababisha maandamano mengi miezi michache iliyopita ambapo wananchi wanaopinga misimamo yake waliandamana hadi katika Ikulu ya White House kuonyesha ghadabu yao.

Kashfa ya hivi majuzi zaidi iliyomwandama Trump, na ambayo ingali inamwandama ni kuhusu jinsi alivyokabili janga la corona nchini humo.

Wakati janga hilo lilipoanza kutikisa ulimwengu, Trump alisisitiza ni homa ya kawaida na kuhimiza watu wasiogope na waendelee na maisha yao kama kawaida bila hata kuvalia barakoa.