Habari

EACC itakunyaka, maseneta waonya Lenku kuhusu kupungua kwa mapato ya kaunti

Na COLLINS OMULO September 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MASENETA wamemuonya Gavana wa Kajiado, Joseph Ole Lenku, kuwa anaweza kuchunguzwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) iwapo serikali ya kaunti itaendelea kupoteza mapato ya ushuru yanayokadiriwa kuwa mamilioni ya pesa.

Hii inajiri baada ya Seneti kuonyesha wasiwasi kuhusu kushuka kwa mapato ya ushuru kutoka kwa vyanzo mbalimbali licha ya kaunti hiyo kuanzisha mfumo wa ukusanyaji ushuru wa kidijitali.

Kamati ya Seneti ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma katika Kaunti ilimkashifu Gavana huyo wa muhula wa pili kwa kuendesha serikali ya kaunti “kama kibanda cha kijijini”.

Ripoti ya mapato ya mwaka wa kifedha ulioishia Juni 30, 2024, ilifichua kwamba mapato kutoka kwa maeneo kadhaa yalishuka kwa kiasi kikubwa, yakiwemo yale ya usimamizi wa maeneo ya hifadhi (Sh33 milioni), matangazo (Sh17 milioni), ushuru wa barabarani (Sh6 milioni), na ada za maegesho (Sh5 milioni), miongoni mwa mengine.

Imebainika kuwa baadhi ya maafisa wa kaunti waliotajwa kuwa waasi wameanzisha nambari zao za malipo ya M-Pesa ambazo hutumika kukusanya ushuru wa kaunti bila kuripotiwa rasmi.

Kulingana na Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA), uwezo wa kaunti ya Kajiado kujikusanyia mapato ni Sh6.8 bilioni, lakini kwa sasa inakusanya Sh1.2 bilioni pekee.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Seneta Moses Kajwang’ (Homa Bay), alisema Gavana Lenku anaongoza mfumo wa ukusanyaji mapato usio na uwazi.

“Tunahisi kuwa mnakusanya pesa lakini hamripoti. Hili linatafsiriwa kuwa ni wizi. Kuna tofauti kubwa katika mapato yenu. Mnawatoza madereva wa malori halafu mnajiwekea pesa?” akauliza Seneta Kajwang’.

“Ikiwa mnachukua pesa kutoka kwa wananchi na kuzitumia nyinyi binafsi, basi huo ni wizi. Tutaomba EACC ifanye uchunguzi iwapo hali hii itaendelea,” akaongeza.

Seneta Samson Cherargei wa Nandi alieleza kuwa kupungua kwa mapato ni mfano dhahiri wa maafisa wa mapato na wale wa utekelezaji kushirikiana kupora mapato ya kaunti.

Seneta wa eneo hilo, Seki Lenku, alisema huenda tatizo likawa katika mfumo wa ukusanyaji mapato au kutowasilishwa kwa ushuru kutoka kwa vizuizi vya barabarani.

Mwaka jana, serikali ya kaunti ya Kajiado ilitangaza kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki kwa asilimia 100 katika ukusanyaji wa mapato ili kuongeza mapato na kuzuia mianya ya ufisadi.

Serikali hiyo ilisema kuwa hatua hiyo ilikuwa na lengo la kuondoa ulipaji wa pesa taslimu katika idara zote, kupunguza nafasi ya wizi na kuongeza uwajibikaji.

Leseni zote za biashara sasa hutolewa mtandaoni, huku malipo yakifanywa kupitia benki au mitandao ya M-Pesa. Hali hiyo pia inahusu leseni za vileo, malipo ya magari ya uchukuzi wa umma na kodi ya vibanda.

Idara ya Ardhi, mojawapo ya vyanzo vikuu vya mapato ya kaunti pia iliunganishwa kikamilifu kwenye mfumo huo.

Usajili wa ardhi, idhini za mipango ya majengo, malipo ya ushuru wa ardhi na kodi sasa hufanywa mtandaoni, hali inayosaidia kupambana na mitandao ya wizi.

Hata hivyo, Gavana Lenku alitetea kupungua kwa mapato, akisema hasa katika ushuru wa usafirishaji, kulisababishwa na hali ya hewa akitaja mvua nyingi iliyovuruga shughuli nyingi.

Wakati wa kikao hicho, kulizuka hali ya sintofahamu baada ya maafisa wa kaunti kukataa kutambua ripoti ya mapato iliyojawa na makosa ya kihesabu na ya kimaandishi.

Ripoti hiyo iliyotaja mapato ya Sh1.2 bilioni ambayo haikutiwa saini na Mkurugenzi wa Mapato wa Kaunti hiyo, Vera Moraa, pamoja na Mkuu wa Kuripoti Mapato, Ken Kulei, ambao walidai ilitayarishwa na mwanafunzi aliyekuwa kwenye mafunzo.

“Hatufai kuendesha kaunti kama vibanda vya kijijini. Kuna suala la zaidi ya Sh1 bilioni, hapa na ni lazima tujue nani wa kubeba lawama,” alisema Seneta Kajwang’.

“Kukataa kusaini ripoti hii ni dalili kuwa wataalamu wanajua kuna matatizo makubwa ndani yake na hawataki kuwajibika,” aliongeza.