EACC kunasa waliopora pesa za Covid
Na MACHARIA MWANGI
MWENYEKITI wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Askofu Mstaafu Eliud Wabukala, amesema uchunguzi kuhusu uporaji wa fedha za kukabiliana na Covid-19 katika Mamlaka ya Kusambaza Dawa (KEMSA) umefikia hatua muhimu.
Askofu Wabukala alisema uchunguzi huo unaendelea vyema na waliohusika na ufisadi huo watakabiliwa vikali kisheria hivi karibuni.
Alifichua kwamba EACC inazichunguza kampuni nane ambazo zilihusika na wizi katika Kemsa.
“Kila mtu ambaye alihusika na ufisadi katika Kemsa ataadhibiwa,” akasema Askofu Wabukala.
Alikuwa akizungumza katika hoteli moja mjini Naivasha baada ya kufungua warsha ya siku tatu kuhusu ufisadi.
Alitaka Kemsa iboreshe utendakazi wake ili kuzuia wizi wa fedha kupitia utoaji wa tenda.
“Baadhi ya wakubwa katika Kemsa ndio hufanya ukora hasa katika utoaji wa zabuni na hushirikiana na wanaopokezwa tenda kwa njia ya ufisadi ili kuifilisi mamlaka hiyo kifedha,” akaongeza Askofu Wabukala.
Alionya kwamba ufisadi ndio umechangia baadhi ya miradi kutokamilishwa kwa wakati na raia kutopata thamani ya ushuru wanaolipa kupitia utekelezaji wa miradi ya umma.
Pia alisema kuwa kuna baadhi ya maafisa wa Mamlaka ya Barabara (KeNHA) ambao hushawishi tenda zitolewe kwa washirika wao kisha hupokezwa fungu baada ya pesa kulipwa.
“Idara ya utoaji wa zabuni ni muhimu sana lakini inaweza kugubikwa na ufisadi, na ndiyo maana inafaa kuongozwa na mtu asiyekuwa na doa la ufisadi,” akasema Askofu Wabukala.
Kwa mujibu wa afisa huyo, tume ya EACC imetwaa mali ya ufisadi yenye thamani ya Sh19.9 bilioni kati ya Sh96 bilioni zilizopotea karne iliyopita.
Mkurugenzi Mkuu wa KeNHA, Peter Mundinia naye alisema kuwa mamlaka hiyo imeziba mianya ya ufisadi.
Alikiri kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikipoteza mabilioni ya fedha kutokana na uharibifu mkubwa wa barabara na malori makubwa.