Habari

EACC yataka Waititu, mkewe kujisalimisha

July 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

JUHUDI za kumsaka Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu pamoja na mkewe waliotoweka kufuatia amri ya kukamatwa kwao iliyotolewa Ijumaa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, zimeshika kasi huku wapelelezi wakiwatia mbaroni washukiwa watatu kuhusiana na sakata ya Sh588 milioni.

Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) imefichua kwamba maafisa wa upelelezi hawakufanikiwa kumkamata Bw Waititu mkewe Susan Wangari Ndung’u na washukiwa wengine watano, na kuwataka kujisalimisha mara moja katika makao makuu ya Tume hiyo kwenye jengo la Integrity Centre, Nairobi.

“Washukiwa wengine wakiwemo Gavana Ferdinand Ndung’u Waititu Babayao, mkewe Susan Wangari Ndung’u, Mhandisi Luka Mwangi Waihenya, Afisa Mkuu wa Wizara ya Barabara na maafisa wengine wa kaunti hawakupatikana katika makao yao wakati uliopangiwa kuwakamata. Tume inawasaka washukiwa hao na inawaagiza kujiwasilisha katika Integrity Center mara moja,” ilisema taarifa ya EACC iliyotumwa kwa vyombo vya habari.

Washukiwa watatu waliotiwa mbaroni ni pamoja na Mkurugenzi wa kampuni ya Testimony Enterprise Bw Charles Chege Mbuthia, wanakamati ya Kutathmini Zabuni Bi Ng’ina Musyoka na Bw Simon Kabocho Kang’ethe, ambao kwa sasa wanazuiliwa katika afisi za EACC.

Bw Waititu ameripotiwa kwenda mafichoni tangu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Bw Noordin Haji atoe amri ya kumkamata mnamo Ijumaa usiku kuhusiana na ufujaji wa fedha za umma za kiasi cha Sh588 milioni.

“Maafisa wamekuwa wakimtafuta katika makao yake lakini hajakuwepo. Hajaonekana tangu Ijumaa usiku, tungali tunamsaka,” afisa wa EACC alisema.

Zabuni

Haya yanajiri siku moja baada ya Bw Haji kuamuru kukamatwa kwa Gavana huyo na mkewe akisema kulikuwa na ushahidi wa kutosha kwamba walipokea kiasi cha zaidi ya Sh25 milioni kupitia kampuni yao ya Saika Two Estate Developers Limited.

Waititu anadaiwa kupokea hela hizo kupitia utowaji wa zabuni kinyume na sheria kwa kampuni ya Testimony Enterprises Limited, iliyopatiwa kandarasi ya kutengeneza barabara za kaunti hiyo.

Washukiwa wengine wanaosakwa na wapelezi ni pamoja na Bi Beth Wangechi Mkurugenzi wa kampuni ya Testimony Limited, Wanakamati wa Kutathmini Zabuni Bw Zecharia Njenga Mbugwa, Bw Anselin Gachukia Wanjiku, na Bw Samuel Muigai Mugo.

Wanakabiliwa na mashtaka kadha yakiwemo: matumizi mabaya ya mamlaka, ukiukaji sheria kimaksudi kuhusiana na ununuzi bidhaa, kujihusisha kibiashara na mali inayotiliwa shaka na mengineyo