Habari

Echesa akabidhi afisi kwa Amina

March 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LEONARD ONYANGO

WAZIRI wa Michezo aliyetimuliwa Rashid Echesa, Jumanne alikabidhi rasmi afisi kwa Amina Mohamed aliyehamishwa kutoka kwa Wizara ya Elimu.

Bw Echesa aliyetimuliwa wiki iliyopita, alikabidhi afisi kwa Bi Mohamed Jumanne asubuhi huku akimshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kumpatia fursa ya kuhudumia Wakenya kwa kipindi cha mwaka mmoja.

“Namshukuru Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto kwa kuniteua kati ya Wakenya milioni 50 kuhudumia taifa hili. Namtakia Bi Amina kila la heri katika wizara ya Michezo na Utamaduni,” akasema Bw Echesa.

Akizungumza siku moja baada ya kuangukiwa na shoka kijijini Marina katika Kaunti ya Kakamega, Bw Echesa ambaye ni mwandani wa Naibu wa Rais, alilalama kuwa hakujua  sababu yake ya kupigwa kalamu.

“Ninawahimiza wafuasi wangu na jamii ya Waluhya kuwa na utulivu. Namshukuru Rais kwa kunipatia fursa ya kuhudumu katika Baraza la Mawaziri,” akasema Bw Echesa.

“Ni jukumu la Rais kuteua na kupiga kalamu mawaziri wake lakini nataka kujua kwa nini nilitumuliwa,” akaongezea.

Ukosoaji

Kutimuliwa kwa Bw Echesa pia kumeshutumiwa vikali na baadhi ya viongozi wa Jubilee hasa wanaoegemea kambi ya Dkt Ruto.

“Hatujafurahishwa na uamuzi wa kumtimua Bw Echesa. Ilikuwa vigumu kueneza sera ya chama cha Jubilee katika ukanda wa Magharibi mwa Kenya. Lakini Echesa alijitolea mhanga kumpigia debe Rais Kenyatta hadi akapata kura nyingi,” akasema mbunge wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali.

Bi Mohamed alihamishwa kutoka wizara ya Elimu hadi wizara ya Michezo huku mwenyekiti wa Baraza la Mitihani nchini (Knec) Prof George Magoha akiteuliwa kuwa waziri wa Elimu.

Kutimuliwa kwa Bw Echesa kumeonekana kuwa pigo kwa naibu wa rais ambaye amekuwa akimtegemea pakubwa katika kuhakikisha kuwa anajipatia uungwaji mkono katika eneo la Magharibi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.