Habari

Elimu ya bure ni hadaa ya serikali – Wazazi

February 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

TITUS OMINDE Na VALENTINE OBARA

POLISI na machifu katika maeneo mbalimbali ya nchi wameimarisha msako wa kukamata wazazi wasiopeleka watoto wao shuleni huku wengi wanaokamatwa wakilalamika kwamba elimu bila malipo iliyoahidiwa na serikali ni ahadi hewa.

Jumatatu katika mahakama ya Eldoret, wazazi watano waliokamatwa walimwambia hakimu kuwa Serikali inadanganya kuwa elimu ya sekondari haina malipo kwani bado wanatakiwa kulipa fedha za chakula, kununua unifomu bali na ada zingine, ambazo walisema hawana uwezo wa kulipa.

Mahakama hiyo iliagiza wazazi hao kutoka kaunti ndogo ya Likuyani, Kaunti ya Kakamega wazuiliwe katika rumande ya gereza la Eldoret hadi Ijumaa baada ya kukiri mashtaka ya kutowapeleka watoto wao shule za upili, baada ya kukamilisha Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) mwaka uliopita.

Wazazi hao waliofikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi wa Eldoret, Bi Christine Menya walikabiliwa na mashtaka ya kukiuka haki ya watoto wao kupata elimu kwa mujibu wa kifungu cha 7 cha Sheria za Watoto.

Lakini walipojitetea, wazazi hao walisema si kupenda kwao kuwanyima watoto wao elimu ya shule za upili bali ni kutokana na ukosefu wa karo na umaskini.

“Mheshimiwa si kupenda kwangu kunyima mtoto wangu haki ya masomo ya shule ya upili. Ukosefu wa karo ndio kizingikiti kikuu katika kutekeleza hitaji hili,” akasema mmoja wao.

Wiki iliyopita, wazazi wanane walikamatwa kwa sababu kukosa kuwapeleka watoto wao shule za upili katika Kaunti ya Taita Taveta.

Ingawa tangu mwaka wa 2008 serikali ilitangaza kuanzisha elimu ya shule za upili za kutwa bila malipo, wazazi bado huhitajika kugharamia mahitaji mengi ya shule kwa watoto wao.

Mwaka uliopita, serikali ilisema kila mwanafunzi aliyefanya KCPE lazima ajiunge na shule ya upili bila kujali alama alizopata na maafisa wa usimamizi serikalini wakaagizwa kuhakikisha hili limetekelezwa kikamilifu.

Wakati mwingi walimu wakuu husema wanalazimika kutoza ada za ziada kutokana na jinsi serikali huchelewa kuwatumia fedha za kugharamia mahitaji ya wanafunzi na pia kiwango cha fedha kinachotumwa huwa hakitoshi.

Katika kesi ya jana, mzazi mwingine aliambia mahakama kuwa kile serikali imekuwa ikisema ni kuwepo kwa elimu ya shule za upili bila malipo ni hadithi tu, kwani bila karo watoto hunyimwa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza.

Hakimu aliamuru kesi hiyo kutajwa Februari 22.