Ena Coach yagongwa kutoka nyuma na trela lililokatika breki Mai Mahiu, wawili wafariki
WATU wawili wamekufa na wengine kadhaa kujeruhuiwa kufuatia ajali iliyohusisha basi la kampuni ya Ena Coach lililokuwa likisafiri kutoka Nairobi kuelekea Kehancha, Kaunti ya Migori.
Ajali hiyo ilitokea Jumamosi usiku katika barabara ya Narok-Mai Mahiu, basi hilo lilipogongwa kutoka nyuma na trela lililodaiwa kupatwa na hitilafu za breki.
Kwenye taarifa Jumapili, Agosti 10, 2025, afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo Richard Mogire alisema kuwa basi hilo, nambari ya usajili KDE 279Q, lilianza safari kutoka Nairobi mwendo wa saa mbili usiku Jumamosi likiwa na abiria 47 na wahudumu watatu.
“Hata hivyo, lilipokuwa likiteremka karibu na Kanisa Katoliki, kisichotarajiwa kilitendeka pale trela moja lilipopatwa na hitilafu za breki na kugonga magari mawili kabla ya kugonga basi hilo kutoka nyuma,” akasema.
“Basi letu lilipoteza mwelekeo na kupinduka kando ya barabara. Kwa huzuni kuu, tunaripoti vifo vya abiria wawili, mwanamke na mtoto. Wengine wengi walipata majeraha,” akaongeza Bw Mogire.
Hata hivyo, duru za polisi zilisema huenda idadi watu waliokufa ikawa zaidi ya watu wawili katika ajali hiyo ya mwendo wa saa tano usiku, Jumamosi.
Bw Mogire aliongeza kuwa makundi ya waokoaji kutoka Shirika la St John Ambulance, Polisi na wahisani walifika haraka katika eneo la ajali na kuwakimbiza hospitalini waliojeruhiwa.
“Tunashukuru kuripoti kuwa wengi wa waliolazwa hospitalini wametibiwa na kuruhusiwa kuondoka. Tunatoa pole zetu kwa familia na marafiki wa wale waliopoteza maisha yao katika ajali hiyo. Aidha, tunawatakia afueni ya haraka waliojeruhiwa,” akaeleza Bw Mogire.