Ethekon aapa hataruhusu wanasiasa kuiba uchaguzi
MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini, Erastus Ethekon, ameapa kwamba chaguzi ndogo zitakuwa huru na kwamba hakutakuwa na visa vya udanganyifu.
Kwa mujibu wa Bw Ethekon hatakubali udanganyifu wowote katika chaguzi ndogo zinazofanyika Novemba 27, 2025 au 2027 na lengo lake ni kurejesha imani ya Wakenya katika tume hiyo.
Alionekana kujibu Muungano wa Upinzani ambao ulikuwa umedai kuwa kuna mpango wa kuiba kura za chaguzi ndogo na uchaguzi mkuu wa 2027.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo Dijitali miezi minne baada ya kuingia afisini, Bw Ethekon alisema hatua ambazo tume hiyo imepiga tayari zinaonekana kwenye kampeni zilizoandaliwa na pia michujo ya vyama kuelekea chaguzi za Novemba 27, 2025
Aliahidi kuwa imani ya Wakenya kwenye utendakazi wa IEBC itaongezeka kutokana na ufanisi ambao umepatikana kwenye chaguzi ndogo za leo.
“Tulirithi shida na jambo la kwanza tulilolifanya ni kuelewa na kufahamu kiini cha shida hiyo. Natumaini nitashirikiana na vyama vya kisiasa, viongozi, mashirika ya kijamii, vyombo vya habari na makundi mengine kufanikisha utendakazi wangu,” akasema Bw Ethekon.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa ufanisi katika chaguzi ndogo za leo na pia 2027 utakuwa ushindi kwa demokrasia na si IEBC.
“Tume haiko debeni, badala yake ni chaguo la Wakenya hasa maeneo ambayo chaguzi ndogo zinaandaliwa,” akasema Bw Ethekon.
Alipuuza madai kuwa maafisa wa IEBC wanashawishiwa na kuingiliwa na serikali akisema kuwa wanachapa kazi kwa kufuata sheria.
“Uaminifu hujengwa kwa siku, miezi au mwaka na huja baada ya wakati fulani lakini kuuvunja huchukua sekunde tu. Kurejesha imani ya Wakenya kwenye tume, tutafanya kazi na kuwajibika kwa kuzingatia sheria,” akasema Bw Ethekon.
Aliwashutumu wanasiasa ambao wamekuwa wakidai kuwa IEBC inapanga kuiba uchaguzi wa 2027 akisema matamshi kama hayo yanalenga tu kuharibu imani ya Wakenya kwenye tume.
“Hakuna mahali wanasiasa hawa wataiba uchaguzi au kuongeza karatasi za kura kwenye masanduku ya kupiga kura. IEBC haishawishiwi kivyovyote au kuingiliwa na mtu yeyote kutoka urais hadi mfagiaji kwa sababu kigezo na nguzo ya utendakazi wetu ni sheria,” akasema Bw Ethekon.
Kauli yake ilikuja wakati ambapo ripoti za ghasia, madai ya IEBC kushirikiana na wanasiasa na kuwepo kwa tashwishi iwapo tume inaweza kuandaa uchaguzi mkuu ambao ni wazi.
Kuelekea uchaguzi mdogo wa Malava, baadhi ya wanasiasa walionekana wakiwapa wapigakura magodoro jambo ambalo lilionekana kama kuwahonga.
Hata hivyo, mkuu huyo wa IEBC alisema kuwa malalamishi pekee waliyoyapata yalikuwa Kasipul ambapo waliwapiga faini Boyd Were wa ODM na Philip Aroko faini ya Sh1 milioni kutokana na ghasia na mauaji yaliyoshuhidiwa wakati wa kampeni kati ya mirengo ya wanasiasa hao.
“Wawaniaji wanaohusika wanastahili kupiga ripoti kwa kufuata utaratibu unaoeleweka ili tuyathibitishe madai hayo. Tusipowasilishiwa malalamishi, basi huwa ni vigumu kuchukua hatua,” akasema.
“Kwa miezi minne ambayo tumekuwa afisini tumetimiza mengi na nina imani kuwa chaguzi za leo zitaendelea vizuri na washindi kupatikana kwa haki,” akasema.
Mwenyekiti huyo pia alikanusha ripoti kwa IEBC inawahangaisha na kuwalemaza vijana wakati huu ambapo usajili wa wapigakura unaendelea. Alisisitiza kuwa vijana wanaendelea kutekeleza wajibu muhimu kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa sababu asilimia 57 ya wale ambao wamejisajili wako kati ya umri wa miaka 28 na 35.