Ethekon akemea wanaodai wataiba kura 2027
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imewataka Wakenya kupuuzilia mbali kuhusu njama ya wizi wa kura ikisema hayana msingi wowote.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumatatu, tume hiyo, ambayo sasa inaongozwa na Erustus Edung Ethekon kama mwenyekiti, ilisema kuwa madai kama hayo ni hatari kwa sababu yanashusha imani ya Wakenya kwa utendakazi wake.
“Matamshi kama hayo, haswa yanayotolewa nje ya kipindi cha uchaguzi hayana msingi, yanayopotosha na yanayoweza kusababisha hofu isiyo na maana yoyote miongoni mwa wananchi,” ikasema IEBC.
“Wakenya wanafaa kuzingatia kwamba IEBC haijatangaza chaguzi zozote. Aidha, hamna tangazo ambalo limechapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali kuhusu suala hilo ili kuchochea kutolewa kwa kauli za kisiasa na propaganda. Huu sio msimu wa kampeni,” ikaongeza tume hiyo.
IEBC imetoa onyo hili baada ya wandani wa Rais William Ruto kutoka eneo la Kaskazini Mashariki kutisha kuwa wataiba kura kumwezesha kiongozi wa taifa kushinda katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Kauli hiyo ilitolewa na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Wajir Fatuma Abdi Jehow aliyeapa kuongoza katika utekelezaji wa uovu huo.
Akiongea wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa na Shule ya Upili ya Wajir, Bi Jehow alifichua kuwa hiyo ni sehemu ya mipango yao ya kuhakikisha Dkt Ruto anapata nafasi ya kuongoza kwa muhula wa pili.
“Kama wabunge kutoka eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya, hatusemi mengi. Kuhusu Rais Ruto tunasema sharti aongoze kwa mihula miwili. Tunasubiri siku ya kura… hata kama kura zetu hazitatosha, tutaiba ili ashinde. Hapo hamna siri,” akasema.
Kauli ya Bi Jehow imeibua kero nchini huku wadau wakipendekeza aadhibiwe kwa kujaribu kuzua uhasama nchini kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.
Lakini IEBC, kwenye taarifa yake ilitaja matamshi ya wanasiasa kama Bi Jehow kama: “Yenye hatari kubwa katika nchi inayozingatia demokrasia kama yetu. Tunahimiza Wakenya kupuuzilia mbali kauli kama hizi na waunga mkono juhudi za kuimarisha kwa demokrasia yetu.”
IEBC iliahidi kushirikiana na wadau, vikiwemo vyama vya kisiasa na viongozi wao ili kujadili njia za kurejesha imani ya Wakenya kwa mchakato wa uchaguzi na matokeo yake.
“Tunatoa wito kwa wadau wote, haswa tabaka la wanasiasa, kukoma kabisa kutoa taarifa au kushiriki vitendo vinavyoweza kudhoofisha imani ya Wakenya kwa uwezo wa tume hii kuendesha uchaguzi kwa njia huru, haki na ambayo matokeo yake yataaminika na wote,” taarifa hiyo ikaeleza.
IEBC ilikariri kuwa itaendesha majukumu yake ya kikatiba kwa njia huru, isiyopendelea na inayozingatia Katiba na sheria husika za uchaguzi.
Tume hiyo ilitaka umma kuthibitisha maelezo kuhusu suala ya uchaguzi kutoka kwa asasi rasmi za IEBC.
Bw Ethekon aliapishwa Ijumaa wiki jana pamoja na wenzake sita.
Wengine ni; Naibu Mwenyekiti Fahima Abdallah, Bi Ann Njeri Nderitu, Bw Moses Alutalala Mukhwana, Bi Mary Karen Sorobit, Bw Hassan Noor Hassan na Profesa Francis Odhiambo Aduol.