Fahari Muadhama Rahim Aga Khan V akipewa Tuzo ya Hadhi zaidi Kenya
MUADHAMA Mwanamfalme Rahim Aga Khan V, Kiongozi wa Waislamu wa Dhehebu la Shia Ismaili Jumanne alipewa Tuzo ya Hadhi zaidi ya Heshima Kenya (Chief of the Order of the Golden Heart of Kenya).
Mwanamflame huyo alipewa tuzo hiyo na Rais William Ruto katika ikulu ya Nairobi ambako viongozi hao wawili waliandaa mazungumzo yaliyojikita katika ushirikiano, uhusiano na miradi ambayo itabadilisha maisha ya mamilioni ya Wakenya.
Kiongozi huyo wa dini aliwasili nchini mnamo Jumatatu jioni. Hii ilikuwa safari yake ya kwanza rasmi Kenya tangu achukue usukani kutoka kwa babake Muadhamu Mwanamfalme Karim Al-Hussaini Aga Khan IV mnamo Februari mwaka huu.
Akiwa ikuluni, Mwanamfalme Zahra Aga Khan pia alipewa Tuzo ya Hadhi ( Elder of Golden Heart) kutoka na uongozi wake bora na kujituma katika kuimarisha sekta za afya, elimu, ustawi wa kijamii Kenya na kote ulimwenguni.
“Mkutano huu ni wa kihistoria na unaonyesha Kenya inathamini sana sifa bora za uongozi wa Ismaili Imamat na miradi ya kijamii. Aga Khan imewezesha Kenya kupiga hatua kwa kuanzisha hospitali, shule na kuwekeza kwenye fani ya uanahabari, sekta za bima, hoteli na kubuni nafasi za ajira,” akasema Rais William Ruto katika ikulu.
Rais pia alieleza imani yake kuwa ushirikiano na Mwanamfalme Rahim utakuwa bora na ule wa kuenziwa kama tu ulivyokuwa enzi za babake.
Aidha alisema miradi ya kuinua jamii inalandana na sera ya serikali ya kuwainua Wakenya wenye mapato madogo maarufu kama ‘Bottom Up’.
Rais pia alitaja ufanisi ambao umepatikana wakati ambapo serikali imekuwa ikishirikiana na Shirika la Maendeleo la Aga Khan (AKDNK).
Alisema zaidi ya wagonjwa 900,000 hutembelea hospitali za Aga Khan kila mwaka ikizingatiwa wana hospitali tatu kubwa nchini kisha zaidi ya vituo 70 vya afya maeneo mbalimbali nchini.