Habari

Familia 700 gizani Lamu

July 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na KALUME KAZUNGU

ZAIDI ya familia 700 kwenye vijiji vya Msafuni, Bomani na baadhi ya maeneo ya Hongwe na Mpeketoni, Kaunti ya Lamu wamekuwa wakiishi gizani kwa zaidi ya miezi miwili kufuatia kuharibika kwa transfoma na hivyo kukatika kwa umeme eneo hilo.

Wakazi waliozungumza na Taifa Leo Jumanne wameilalamikia kampuni ya kusambaza umeme nchini kwa kukosa kuwajibikia tatizo hilo na badala yake kuwaacha wateja wao wakihangaika kwa kipindi kirefu.

Mkazi wa Msafuni Bw Jonathan Kamau, alisema licha ya kuwasilisha kilio chao mara kwa mara kwa ofisi za kampuni hiyo, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa hadi sasa kurekebisha tatizo hilo.

Bw Kamau alisema tangu umeme kukatika eneo hilo, visa vya wizi barabarani na mitaani vimekithiri mno kwani wezi wamekuwa wakitumia mwanya huo kutekeleza uovu wao.

“Tumekuwa tukiisukuma kampuni kurekebisha tatizo hilo bila mafanikio. Ni karibu mwezi wa tatu sasa umeingia tangu umeme kukatizwa eneo hili. Kila unapolalamika unaambiwa ni transfoma ndizo ziliungua. Kwa nini wasilete transfoma mpya na kurekebisha tatizo la ukosefu wa stima maeneo yetu? Huo ni utepetevu wa hali ya juu,” akasema Bw Kamau.

Mwakilishi wa Wadi ya Hongwe, James Komu, alitisha kuishtaki kampuni kwa kuwasababishia wakazi hasara ya kukosa stima kwa muda mrefu kupita kiasi.

Alisema baadhi ya maeneo kama vile Bomani yameachwa bila stima kwa kipindi cha takriban miezi sita.

“Baadhi ya transfoma kama ile ya kijiji cha Bomani ziliungua karibu miezi sita iliyopita na hadi sasa hazijarekebishwa au kubadilishwa. Wakazi, ikiwemo wanabiashara wamekuwa wakikadiria hasara kubwa kwa kipindi chote cha miezi sita ya kukosa stima. Lazima Kenya Power ifidie hawa watu wetu na pia ibadilishe transfoma na kuileta mpya,” akasema Bw Komu.

Kwa upande wake, Meneja wa Mauzo wa Kenya Power tawi la Lamu, Bernard Kataka, amethibitisha kuwepo kwa tatizo hilo na kufichua kuwa wamekuwa wakikumbwa na tatizo la kupata na kununua aina hiyo ya transfoma iliyoharibika.

Alisema kampuni inajitahidi kutafuta tranfoma mpya ili kurekebisha tatizo hilo ambalo limewaacha wananchi wengi gizani.

“Ni kweli. Kumekuwa na tatizo la kukatizwa kwa stima kwenye vijiji husika. Transfoma nyingi ziliungua lakini aina hiyo ya transfoma ni vigumu kuipata. Hata hivyo tuko mbioni ili kupata tranfoma hizo na kurekebisha tatizo lililoko kufikia mwishoni mwa juma hili,” akasema Bw Kataka.