Habari

Familia ya aliyekufa seli yakataa ripoti ya upasuaji maiti

Na MWANGI MUIRURI  August 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

FAMILIA ya Stephen Mwangi mwenye umri wa miaka 35, ambaye Huduma ya Kitaifa ya Polisi inadai alijitia kitanzi katika Kituo cha Polisi cha Kenol, imekataa matokeo ya upasuaji wa maiti.

Matokeo hayo yaliyotolewa na Dkt Waithera Mbau, Jumatatu katika mochari ya Hospitali ya Murang’a Level Five, yalieleza kuwa Mwangi alifariki kutokana na kukosa hewa.

Hata hivyo, Dkt Mbau alifafanua kuwa ripoti hiyo haikuwa ya mwisho kwa kuwa vipimo zaidi vya kimaabara vinahitajika ili kubaini chanzo halisi cha kifo.

Msemaji wa familia, Bw Julius Ngugi, alieleza kutoridhishwa na ripoti hiyo.

“Tumeshangaa kwamba upasuaji huo haukuangazia baadhi ya dalili muhimu. Wakati wa kuutazama mwili katika mochari mnamo Agosti 12, 2025, ulikuwa ukitoka damu mdomoni,” alisema.

Hata hivyo, Dkt Mbau alisema hakuona majeraha yoyote ya nje kwenye mwili huo.

Familia ilipinga hilo kwa kudai kwamba damu hiyo ilionyesha kuwepo kwa uvujaji wa ndani, aidha kichwani au shingoni.

Lakini daktari huyo alisema hakuona dalili zozote za majeraha.

“Hakukuwa na majeraha kwenye misuli ya shingo wala damu chini ya ngozi,” alieleza kwenye ripoti yake.