Habari

Familia ya dabo dabo

November 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

WAZIRI wa Leba Ukur Yattani na mkewe Dkt Gumato Yattani, wameingia katika madaftari ya kumbukumbu kwa kuwa watu wa familia iliyobarikiwa, kwa kupata nyadhifa mbili kuu kila mmoja katika serikali.

Ijumaa, Dkt Yattani aliteuliwa kufanya kazi katika mashirika mawili tofauti, sawa na mumewe ambaye anashikilia Wizara ya Fedha tangu aliyekuwa waziri, Henry Ritoch aliposimamishwa kazi kuhusiana na tuhuma za ufujaji fedha za umma.

Kwenye tangazo katika Gazeti Rasmi la Serikali, Dkt Yattani aliteuliwa na waziri wa elimu Prof George Magoha kuwa mwenyekiti wa Bodi Simamizi ya Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT).

Naye waziri wa Ustawi wa Viwanda, Bw Peter Munya akamteua kuwa miongoni mwa wale watakaohudumu katika Jopo Maalum Kuhusu Miundomsingi Bora Nchini.

Uteuzi huo unajiri huku maelfu ya vijana nchini wakiendelea kuilaumu serikali kutokana na ukosefu wa ajira. Kwenye kampeni zake za urais kupitia chama cha TNA na baadaye Jubilee, Rais Uhuru Kenyatta alikuwa ameahidi kubuni nafasi za kazi kwa vijana. Lakini ahadi hiyo yamkini imetupwa kwenye jaa, huku wazee na watu wa familia chache zenye ushawishi wakiendelea kula minofu serikalini.

Rais Kenyatta amekuwa akilaumiwa kwa kuwapuuza vijana kwenye teuzi kuu serikalini, licha ya kuahidi kubuni nafasi za ajira kwao kwenye kampeni yake mnamo 2017.

Miongoni mwa wazee wanaohudumu serikalini ni aliyekuwa Makamu wa Rais Moody Awori, 92, na aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Bw Francis Muthaura, aliye na umri wa miaka 73.

Familia ya waziri Yattani ambaye amekuwa serikalini awali kama mkuu wa wilaya (DC), Balozi, kabla ya kuingia bungeni kuwakilisha eneo bunge la North Horr imeangaziwa na nyota ya jaha. Mnamo 2013, alichaguliwa kuwa gavana wa kwanza wa Marsabit na sasa ni waziri wa Leba na pia Fedha.

Kwenye uteuzi wa Ijumaa, aliyekuwa Mhariri Mkuu katika Shirika la Habari la Nation (NMG) Bw Tom Mshindi na aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) Bw Gabriel Lengoiboni pia waliteuliwa kuwa wanachama wa bodi ya kusimamia Chuo Kikuu cha JKUAT.

Kilichoshangaza zaid, ni kuteuliwa kwa Seneta wa Uasin Gishu, Prof Margaret Kamar kuwa mwanachama wa Hazina ya Kitaifa ya Walemavu (NFDK). Wanachama wengine walioteuliwa kwenye bodi hiyo ni Bi Cecilia Mbaka na Bi Anne Mugambi.

Aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Kike Kaunti ya Kwale, Bi Zainab Chidzuga naye aliteuliwa kuwa mwanachama wa Bodi ya Kusimamia Maeneo Maalum ya Uzalishaji (SEZA).

Mutahi Kagwe

Wakati huo huo, serikali imefutilia mbali uteuzi wa aliyekuwa Seneta wa Nyeri Bw Mutahi Kagwe kuwa mwanachama wa Bodi ya Kusimamia Kawi (EPRA).

Kulingana na Waziri wa Kawi Bw Charles Keter, nafasi yake itachukuliwa na aliyekuwa Mwanasheria wa Serikali Bw Wanjuki Muchemi.

Bw Keter hakutoa sababu yoyote ya kufutiliwa mbali kwa uteuzi huo.