Habari

Familia ya Kibaki yadai utajiri wake ni Sh50 milioni tu

Na JOSEPH WANGUI  May 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MALI ya rais wa zamani Hayati Mwai Kibaki na thamani yake inapigwa darubini mahakamani katika kesi inayohusisha wana wake wanne na watu wengine wawili wanaotaka kutambuliwa kama warithi wa mali hiyo.

Lakini familia yake ikiongozwa na Bi Judith Wanjiku, imewasilisha kesi mahakamani kuonyesha kuwa Kibaki aliacha mali ya thamani ya Sh50 milioni.

Hii ni baada ya mmoja wa walalamishi, aliyetambuliwa kama JNL, kuwasilisha stakabadhi fulani mahakamani zinazoonyesha rais huyo wa zamani alikuwa bilionea.

Kibaki alikufa katika Nairobi Hospital Aprili 22, 2022 akiwa na umri wa miaka 90. Aliacha wosia alioandika Desemba 23, 2016 akielezea jinsi angetaka mali yake igawanywe kwa warithi wake.

Bi JNL anasema katika uchunguzi wake aligundua kuwa Kibaki alikuwa mmiliki na mshirika wa angalau kampuni sita za kibiashara na uwekezaji.

Miongoni mwa washirika wake kibiashara ni pamoja na Kenneth Matiba, Chris Kirubi, Joseph Gethenji na Charles Mwangi Gathuri.

Kampuni hizo ni pamoja na International House Limited, Pinpoint Investments Limited, Farmlands Company Limited, Kentrout (1972) Limited, Gingalili (1968) Limited na Lucia and Company Limited.

Katika kampuni hizo, Kibaki alikuwa mkurugenzi na mmiliki mkuu wa hisa.

Stakabadhi za Bi JNL alizozipata kutoka kwa Msajili wa Kampuni, zinaonyesha kuwa Kibaki alimiliki kampuni ya Farmlands Limited na wenye hisa wengine saba akiwemo Bw Gethenji, ambaye ni baba wa Mbunge wa zamani wa Tetu- kupitia Wain Limited na Wagema Limited.

Bw Gethenji ni babake James Ndung’u Gethenji ambaye alihudumu kama Mbunge wa Tetu kati ya 2017 hadi 2022.

Wenye hisa wengine ni marehemu Bw Matiba (kiongozi wa zamani wa upinzani) Francis Mwai na marehemu Margaret Wanjiku.

Kulingana na JNL, Kampuni nyingine ya uwekezaji ambayo Kibaki alimiliki na wengine ni Kentrout. Wengine waliomiliki hisa katika kampuni ni aliyekuwa mfanyabiashara mashuhuri marehemu Mwangi Gathuri.

Bi JNL pia anasema kuwa Kibaki alimiliki jumba la International House, lililoko katikati mwa jiji la Nairobi, pamoja na marehemu Kirubi na wengine.

Alimiliki idadi kubwa ya hisa za kampuni ya International House Limited, iliyosajiliwa rasmi Mei 1985 kusimamia jumba hilo, kulingana na stakabadhi kutoka kwa msajili wa kampuni.

Bi JNL pamoja na Jacob Ocholla, walipinga kupewa kibali kwa Bi Wanjiku asimamie wosia wa Kibaki na ugavi wa mali yake.

“Nilielekea kortini kwa sababu nilitengwa kama mrithi wa mali ya Kibaki na kwa sababu, Judith Wanjiku, James Mark Kibaki, David Kagai na Anthony Andrew Githinji walihadaa mahakama kuhusu thamani halisi ya marehemu babangu,” anasema.

Huku akiwasilisha ombi kwamba aruhusiwe kusimamia wosia na mali ya Kibaki, Bi Wanjiku alisema kuwa mali ya Kibaki inayojulikana ni vipande saba vya ardhi vilivyoko Othaya na Nyeri vyenye thamani ya Sh50 milioni.

Hakuwa na madeni yoyote.

Utata umegubika thamani halisi ya mali ya Kibaki kwa sababu katika stakabadhi ya wasia, ambayo ni sehemu ya stakabadhi zilizowasiliswa kortini, hakuorodhesha mali ambayo angetaka irithiwe.

Aliorodhesha watoto wake wanne kama wasimamizi wa wosia huo.Kwa mfano, wosia unasema bila kutoa maelezo, kwamba aliwarithisha wanawe pesa zilizokuwa kwenye akaunti ya benki.

Alitaka pesa hizo zigawanywe kwa usawa miongoni mwa wanawe.