Familia yaingiwa na wasiwasi kijana wao shabiki wa Man U akitoweka
FAMILIA moja imeingiwa na wasiwasi baada ya mwanao aliyekuwa ametoka kutazama mpira wa soka ya Ligi Kuu Uingereza kutoweka mnamo Januari 19.
Vincent Oluoch Omondi alitoweka mnamo Januari 19, baada ya kutazama Manchester United ikipoteza 3-1 dhidi ya Brighton.
Japo alikuwa shabiki wa Manchester United, Bw Oluoch hakuoneka kama mwenye ghadhabu kutokana na matokeo hayo kwa kuwa timu hiyo imekuwa na mkondo mbaya wa matokeo.
![](https://d1qw3p19ag2ajj.cloudfront.net/uploads/2025/02/DNMISSINGPERSON0602H2.jpg)
Alirejea nyumbani kijiji cha Kisii, mtaani South B saa mbili usiku kisha akaondoka akiwacha simu yake ikipashwa moto.
“Nimeacha simu ikipata moto, nitarudi,” akasema, mkewe Saida Nakahoya asijue hayo ndiyo maneno yake ya mwisho,
Bw Oluoch, 27 aliondoka kwenye boma lake bila kuwa na ugomvi wowote na mkewe.
Baada ya saa mbili kupita, Bi Nakahoya aliingiwa na wasiwasi mumewe alipokosa kurudi huku chajio alichokuwa amemwaachia kikiingia baridi.
Alikuwa na matumaini kuwa mumewe bado alikuwa akipiga gumzo na marafiki zake kuhusu soka mita chache kutoka ukumbi ambako walikuwa wakitazama mpira.
Hadi leo, mumewe bado hajarejea huku suala hilo likimkosesha usingizi akiwa na mtoto mwenye umri wa miezi miwili na wiki moja pekee.
“Tangu siku hiyo sijamwona na naomba sana apatikane kwa sababu sasa nalaumiwa kuhusu hali hii,” akasema Bi Nakahoya akiongea na Taifa Leo.
Kile ambacho anakumbuka ni kuwa Bw Omondi alikuwa amemgusia aligombana na wafanyakazi wenzake mahali anapofanya kazi barabara ya Baricho, Nairobi. Hata hivyo, hakutoa ufafanuzi wa kina kuhusu suala hilo.
Paul Oduor, mjombake Bw Oluoch alisema wametembelea hospitali na vituo vyote vya polisi wakitarajiwa kumpata mpwa wake. Mnamo Januari 21 walipiga ripoti kuhusu kutoweka kwake katika kituo cha polisi cha South B chini ya nambari ya OB 17/21/01/2025.
![](https://d1qw3p19ag2ajj.cloudfront.net/uploads/2025/02/DNMISSINGPERSON0602C.jpg)
“Tumetembelea hospitali ya Kenyatta na makafani ya City na hata kueleza DCI. Tumetembelea pia vituo vya polisi nje ya Nairobi lakini hatujampata,” akasema Bw Oduor.
Vijana wamekuwa wakitoweka ikidaiwa huwa wanakosoa serikali lakini Bw Oduor anasema mpwa wake hakuwa akijihusisha na siasa kwa sababu alikuwa akimakinikia soka pekee.
“Hatuwezi kusema kutoweka kwake kunahusiana na kukosoa serikali ila tunaiomba serikali itusaidie kumpata. Hilo tu litatupa faraja,” akaongeza.
Nduguye Stephen Otieno Omondi na marafikize aliokuwa akitazama nao mechi ya Man United dhidi ya Brighton walisema wamesikitishwa na kutoweka kwake.